• HABARI MPYA

  Sunday, June 26, 2016

  TFF YAWAONYA YANGA; "MKIWAGUSA AZAM TV MNAONDOLEWA KWENYE MASHINDANO"

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limeionya klabu ya Yanga iwapo itawafanyia fujo warusha matangazo wa Televisheni ya Azam, wanaweza kuodolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.
  Tahadhari hiyo inafutaia taarifa za mpango na kauli za baadhi ya viongozi wa Yanga SC kushawishi mashabiki wao kufanya vurugu dhidi ya warushaji matangazo ya televisheni ya moja kwa moja wakati wa mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho la Afrika dhidi yao na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Jumanne Uwanja wa Dar es Salaam.
  Mashabiki wa Yanga wanatakiwa kuwa watulivu Jumanne na wasiwafanyie fujo Azam TV

  Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas amesema katika taarifa yake; "TFF ikiwa msimamizi mkuu wa mpira wa miguu Tanzania, inawajibika na mara moja inachukua nafasi hii kuwatahadharisha baadhi ya viongozi wa Young Africans, wanachama na mashabiki wao kutofanya hivyo kwani itakuwa ni kinyume na  kanuni za mashindano na mikataba ya udhamini katika hatua hii,".
  "Ikumbukwe kwamba CAF inamiliki asilimia mia moja ya haki za habari na masoko katika ngazi hii ya makundi na jaribio lolote la kukwamisha matangazo ya biashara au utengenezaji na urushaji wa matangazo ya televisheni au ukwamishaji wa shughuli zingine kama hizo kwa CAF au wakala aliyeteuliwa na CAF kutaigharimu klabu mwenyeji si kwa kutozwa faini tu lakini pia uwezekano wa kuondolewa mashindanoni,".
  "Pia TFF inatoa tahadhari hiyo ikiwamo ile ya utamaduni wa kukaa uwanjani ili kuepusha aina yoyote ya vurugu kwenye michezo yake hususani hii ya hatua ya makundi. TFF inafahamu kuwa tayari viongozi wa Yanga walikwisha kusoma nyaraka na taarifa mbalimbali kuhusu kanuni na masuala ya udhamini kwa timu zinazofuzu hatua ya Nane Bora,".
  "Wapenzi wa Yanga wanaombwa kufika kwa wingi na kuishangilia kwa nguvu  timu yao ikiwa ni njia ya kuitia hamasa.Hata hivyo shamrashamra hizo zifanyike kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu za Mpira wa Miguu na sheria za nchi,".
  "Vitendo vya kuashiria vurugu na kufanya vurugu vikithibitishwa katika taarifa ya Mwamuzi, Janny Sikazwe wa Zambia; Kamishna wa mchezo, Celestin Ntangungira wa Rwanda na Mratibu Mkuu Maalumu kutoka Msumbiji, Sidio Jose Mugadza, hatua zake zitachukuliwa dhidi yake ikiwamo KUONDOLEWA KWENYE MASHINDANO,". 
  Vilevile vitendo vya kutishia amani,kudhuru mwili au kuharibu mali vitachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za kijinai.
  Katika mchezo huo wa kimataifa Na. 107, Mwamuzi Sikazwe atasaidiwa na Jarson Emiliano dos Santos kutoka Angola atayekuwa kwenye mstari wa kulia (line 1) na Berhe O’Michael wa Eritrea atayekuwa upande wa kushoto (line 2) huku Wellington Kaoma wa Zambia akiwa ni mwamuzi wa akiba,".
  Wakati huohuo, kikao cha Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini kinatarajia kukaa siku ya Jumamosi tarehe 2 Julai 2016. Taarifa zaidi itatolewa karibuni,".
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF YAWAONYA YANGA; "MKIWAGUSA AZAM TV MNAONDOLEWA KWENYE MASHINDANO" Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top