• HABARI MPYA

  Jumapili, Juni 26, 2016

  SIMBA SC INAVYOJIANDAA KUENDELEA KUWA ‘YA MATOPENI’

  UONGOZI wa Simba SC upo kwenye mchakato wa usajili kwa ajili ya kikosi cha msimu ujao – baada ya kuwa na misimu mitatu mibaya iliyopita.
  Wachezaji watatu wamekwishasajiliwa kati ya 33 waliopendekezwa na Kamati ya Ufundi ya Simba SC, chini ya Mwenyekiti Collin Frisch ambao ni beki Emmanuel Semwanza kutoka Mwadui FC na viungo Muzamil Yassin na Mohammed Ibrahim kutoka Mtibwa Sugar.
  Orodha ya wachezaji 33 waliopendekezwa na Kamati ya Ufundi ilipelekwa kwenye Kamati ya Utendaji na kupunguzwa hadi kupata orodha fupi ya wachezaji wa kusajiliwa.
  Na bila shaka usajili huu unaovuja ndiyo ambao unatokana na orodha ya mwisho iliyopitishwa na Kamati ya Utendaji, chini ya Rais wa klabu, Evans Aveva.
  Wakati huo huo; Simba ipo katika mchakato wa kutafuta kocha Mkuu, ambaye labda atafanya kazi na kocha aliyemaliza msimu na timu, Mganda Jackson Mayanja.
  Lakini kocha anayetajwa kuja Simba ni Mcameroon, Joseph Marius Omog ambaye misimu miwili iliyopita alikuwa Azam FC.
  Hakuna uhakika kama Omog atakubali kufanya kazi chini ya Mganda Mayanja – hususan kutokana na kumbukumbu zake alipofanya kazi na Mganda mwingine, George Nsimbe alipokuwa Azam.
  Omog aliondolewa kazini na Nsimbe aliyekuwa Msaidizi akawa kaimu kocha Mkuu, kabla ya naye kuondolewa na kurejeshwa Muingereza Stewart Hall, aliyejiuzulu mwishoni mwa msimu.
  Kama Omog atauchukulia ni usaliti aliofanyiwa na Nsimbe walipokuwa Azam, hatakuwa na imani na kocha mwingine Mganda. Siombi iwe hiyo, naomba waelewane na wafanya kazi pamoja. 
  Lakini pamoja na yote, atakapowasili Omog Simba SC atakuta wachezaji wamekwishasajiliwa naye aanze kuandaa timu kwa ajili ya msimu mpya.
  Misimu miwili, mitatu iliyopita tumeshuhudia desturi hii ya Simba kusajili wachezaji kabla ya makocha ikileta mushkeli na kwa kiasi kikubwa imechangia matokeo mabaya ya timu.
  Makocha wanapoingia Simba wamekuwa hawakubaliani na aina ya wachezaji waliosajiliwa na kuomba muda wamalize msimu timu ibaki Ligi Kuu, ili wasajili aina ya wachezaji wawatakao.
  Lakini mwishoni mwa msimu makocha hao wamekuwa wakifukuzwa na viongozi wanasajili tena wachezaji na kuleta kocha baadaye.
  Na sasa inaelekea kuwa hivyo hivyo – Aveva amekwishaanza kusajili na baadaye atafautia Omog aje kufundisha wachezaji waliosajiliwa na Rais.
  Hata kabla Omog hajawasili nchini kusaini Mkataba. Hata kabla Simba haijaanza maandalizi ya msimu mpya. Hata kabla ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara haijaanza tayari unaweza kuanza kupata picha Simba inalekea wapi msimu ujao.
  Inaelekea kurudia kufanya kile ambacho imekuwa ikifanya kwa misimu mitatu iliyopita – kukosa mataji na kuendelea kuitwa ‘wa matopeni’ na mahasimu wao, Yanga.
  Umefika wakati sasa viongozi wa Simba wabadilike – au wajifunze kutokana na makosa waliyoyafanya kwa misimu iliyotangulia.
  Haiwezekani wasajiliwe wachezaji kabla ya kocha. Mapema tu Januari mwaka huu Simba ilijua imeingia kwenye kipindi cha mpito, baada ya kuachana na kocha Muingereza Dylan Kerr.
  Ni wakati ule Simba ilipaswa kuleta kocha ambaye angeanza kuifuatilia timu ikiwa chini ya kocha Mayanja na kuona mapungufu yake.
  Baada ya msimu angeketi mezani na uongozi na kujadiliana nao namna ya kujenga timu mpya kuelekea msimu mpya.
  Namna hii viongozi wa Simba wataendelea kugombana na wachezaji, wataendelea kufukuza makocha na wataendelea kukosa mataji.  Na wataendelea kuitwa ‘Wa Matopeni’ na mahasimu wao, Yanga. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC INAVYOJIANDAA KUENDELEA KUWA ‘YA MATOPENI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top