• HABARI MPYA

  Jumatano, Juni 29, 2016

  ULIMWENGU AISHAURI YANGA CHA KUFANYA IFIKE NUSU FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa TP Mazembe, Mtanzania Thomas Emmanuel Ulimwengu amesema kwamba Yanga inaweza kufika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho mwaka huu iwapo itamalizia vizuri mechi zilizobaki.
  Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) jana iliifunga Yanga bao 1-0 katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Hicho kinakuwa kipigo cha pili mfululizo kwa Yanga, baada ya Juni 19 kufungwa pia 1-0 na wenyeji MO Bejaia 1-0 nchini Algeria.
  Na baada ya ushindi huo uliotokana na bao la Mereveille Boppe aliyemalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Chrtistian Luyindama dakika ya 74, Ulimwengu amesema Yanga si timu mbaya, ila kama inataka kufika mbali, ijirekebishe.
  Thomas Ulimwengu amesema Yanga inaweza kufika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho mwaka huu iwapo itamalizia vizuri mechi zilizobaki

  Ulimwengu amesema kwamba Mazembe ni timu bora mbele ya Yanga na nyingine zote katika kundi hilo, zikiwemo Medeama ya Ghana na MO Bejaia ya Algeria.
  Na Ulimwengu amesema anaamini wote Yanga, MO Bejaia na Medeama wanawania kuungana na Mazembe kwenda Nusu Fainali.
  “Kwa hiyo sasa kama Yanga wanataka kuungana na sisi kwenda Nusu Fainali, lazima wafanyie kazi mapungufu yao, kwa sababu hao washindani wao (Medeama na Bejaia) ni wazuri pia. Sisi tumecheza na Medeama nyumbani (Lubumbashi), ndiyo tumewafunga 3-1, lakini walicheza vizuri, ni timu nzuri,”alisema.
  Ulimwengu amesema Yanga bado ina nafasi ya kufika Nusu Fainali iwapo tu kocha wake, Mholanzi Hans van der Pluijm atarekebisha makosa ya timu na kushinda mechi zote zilizobaki.
  Katika mchezo huo ambao mashabiki waliingia bure, Mazembe walionyesha kiwango kikubwa zaidi ya Yanga kuashiria kwamba walistahili ushindi huo.
  Shambulizi la maana la Yanga lilikuja dakika ya 44 tu baada ya mshambuliaji Mzimbabwe kufanikiwa kumzidi mbio na maarifa beki Luyindama na kumpasia kiungo Deus Kaseke aliyepiga nje akiwa amebaki na kipa, Sylvain Gbohouo Guelassiognon.
  Kipindi cha pili, Mazembe walifunguka zaidi na kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Yanga hadi kupata bao lao pekee.
  Yanga itahitimisha mechi zake za mzunguko wa kwanza za Kundi A kwa kucheza na Medeama ya Ghana Agosti 7 Uwanja wa Taifa pia.
  Watacheza mechi ya mwisho ya nyumbani na MO Bejaia kabla ya kusafiri kwenda Ghana na baadaye Kongo kumalizia mechi za kundi lao ili kuangalia mustakabali wao wa kwenda Nusu Fainali.
  Kwa sasa, Mazembe yenye pointi sita inaongoza kundi hilo, ikifuatiwa na Mo Bejaia yenye pointi tatu ambayo leo inamenyana na Medeama ambayo haina pointi kama Yanga kukamilisha mzunguko wa pili wa kundi A.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ULIMWENGU AISHAURI YANGA CHA KUFANYA IFIKE NUSU FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top