• HABARI MPYA

    Wednesday, June 29, 2016

    HIVI WANA YANGA WANAMUELEWAJE MANJI!

    YANGA jana imemaua mashabiki wake waingie bure katika mchezo dhidi ya TP Mazembe ya DRC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga ilifungwa 1-0, bao pekee la Mereveille Boppe aliyemalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Chrtistian Luyindama dakika ya 74.
    Hicho kinakuwa kipigo cha pili mfululizo kwa Yanga katika hatua ya makundi, baada ya Juni 19 kufungwa pia 1-0 na wenyeji MO Bejaia 1-0 nchini Algeria.
    Bila shaka huwezi kusumbua kichwa kujiuliza Yanga wamepata wapi jeuri ya kuingiza mashabiki bure, wakati iko wazi ni Mwenyekiti wake, bilionea Yussuf Manji.
    Manji ndiye anaendesha Yanga kwa fedha zake za mfukoni na hajali klabu inaingiza kiasi kidogo, yeye anasajili wachezaji wa bei kubwa, anawapa mishahara mikubwa na posho nzuri.
    Anawapeleka kambini Uturuki kujiandaa na mechi zake na wakirudi nyumbani, anawaweka hoteli ya nyota tano.
    Na hicho ndicho Yanga walimpendea Manji wakaamua kumchagua kwa awamu ya pili katikati ya mwezi huu kuendelea kuwa Mwenyekiti wao kwa miaka mingine minne.
    Wanaona kabisa timu yao ipo kwenye mikono salama chini ya Manji na alichokifanya jana hakuna ambaye angeibuka kupinga kwamba klabu inapoteza fedha.
    Mechi kubwa kama hizi haziji mara kwa mara na zinapotokea zinakuwa za kihistoria na klabu nyingine hupenda kuweka hata rekodi za mapato.
    Lakini kwa Manji halikuwa na umuhimu hilo – aliamua kuwapa ahueni wana Yanga wote waende kwa wingi Uwanja wa Taifa kuishuhudia timu yao na kuishangilia.
    Yanga iliingia katika mchezo wa jana ikitoka kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa kukodi wa Gymkhana na baada ya mchezo huo sijui itakwenda kukodi Uwanja wa Loyola au Karume.
    Yanga haina Uwanja wake wa mazoezi na Manji hadi leo hajawapatia jibu la kueleweka wanachama wa timu hiyo kwa nini anashindwa kuifanyia hilo dogo klabu.
    Kujenga Uwanja kwa ajili ya mechi, labda hilo ni kubwa sana na linahitaji fedha nyingi, lakini kuipatia klabu tu Uwanja wa mazoezi, Manji hawezi kuwa na kisingizio, labda aseme hajaamua tu.
    Manji anafanya mambo makubwa sana ya gharama kubwa Yanga kuliko kuijengea Uwanja wa klabu. Najiuliza kwa nini?
    Anaingia gharama kubwa kulipia viwanja vya kukodi kila siku – lakini angeweza kutumia kiasi cha Sh. Milioni 30 tu kuifanya Yanga iwe na Uwanja wake wa mazoezi.
    Yanga ingeweza kununua eneo kubwa nje ya mji na kuotesha nyasi, wakapata Uwanja mzuri wa mazoezi. 
    Hilo Manji anaweza – lakini kuona siku zinakatika Yanga haina Uwanja wake wa mazoezi tu nashindwa kumuelewa Manji.
    Na ninashindwa kumuelewa kwa sababu gharama anazotumia kwa matumizi yasiyo ya lazima Yanga ni kubwa kuliko gharama za kuifanya Yanga iwe na Uwanja wake wa mazoezi tu.
    Kwa mimi ni hivyo, ila sijui kwa Yanga wenyewe wanamuelewaje Manji kaika hili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HIVI WANA YANGA WANAMUELEWAJE MANJI! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top