• HABARI MPYA

  Jumatano, Juni 22, 2016

  OSCAR JOSHUA AANZA KULIPIGA JARAMBA UTURUKI, CHIRWA NAYE AFANYA MAZOEZI

  Na Prince Akbar, ANTALYA
  BEKI wa kushoto wa Yanga, Oscar Joshua Fanuel leo ameanza mazoezi mepesi katika kambi ya timu hiyo mjini Antalya, Uturuki kujiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe wiki ijayo.
  Yanga itawakaribisha Mazembe Jumanne ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huo ukiwa mchezo wa pili wa Kundi A, baada ya Jumapili kufungwa 1-0 na wenyeji Mouloudia Olympique Bejaia Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia Jumapili.
  Katika mchezo huo, Oscar aliumia kipindi cha kwanza na kushindwa kuendelea nafasi yake ikichukuliwa na Mwinyi Hajji Mngwali ambaye bahati ambaye naye akaonyeshwa kadi mbili mfululizo za njano na kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 90.
  Oscar Joshua ameanza mazoezi mepesi leo kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya TP Mazembe Jumanne

  Kambi ya Yanga ikaingiwa na hofu ya kuingia kwenye mchezo na Mazembe bila beki halisi wa kushoto kutokana na Oscar kuwa majeruhi na wakati huo huo Mwinyi anatumikia adhabu ya kadi.
  Hata hivyo habari njema ni kwamba Oscar leo ameanza mazoezi mepesi na Daktari Edward Bavu anaendelea kufuatilia hali yake kwa karibu.  
  Wakati huo huo, winga mpya wa Yanga, Mzambia Obrey Chirwa naye leo ameanza mazoezi baada ya kuwasili akitokea Dar es Salaam alikorejea mara moja kushughulikia uhamisho wake.
  Chirwa aliyesajiliwa wiki iliyopita kutoka FC Platinums ya Zimbabwe anatarajiwa kupewa nafasi katika mchezo dhidi ya Mazembe Jumanne Dar es Salaam.
  Usajili wa mchezaji huyo ni mapendekezo ya wachezaji wengine wa Yanga iliyowasajili kutoka Platinums msimu ulkiopita, Wazimbabwe kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliajin Donald Ngoma.

  Winga Mzambia Obrey Chirwa ameanza mazoezi leo kambini Antalya

  Kikosi kamili cha Yanga kilichopo kambini Uturuki ambacho kinatarajiwa kurejea Ijumaa usiku ni makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benno Kakolanya.
  Mabeki; Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Vincent Bossou na Nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro'.
  Viungo; Thabani Kamusoko, Juma Mahadhi, Said Juma ‘Makapu’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Godfrey Mwashiuya na Obrey Chirwa.
  Washambuliaji; Donald Ngoma, Matheo Anthony na Amissi Tambwe.
  Msafara upo chini ya Kocha Mkuu, Mholanzi, Hans van der Pluijm, Kocha Msaidizi Juma Mwambusi, Kocha wa makipa, Juma Pondamali, Daktari Edward Bavu, Mchua Misuli, Jacob Onyango, Mtunza Vifaa Mohammed Mpogolo na Meneja Hafidh Saleh. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: OSCAR JOSHUA AANZA KULIPIGA JARAMBA UTURUKI, CHIRWA NAYE AFANYA MAZOEZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top