• HABARI MPYA

  Sunday, June 26, 2016

  SERENGETI BOYS YAITANDIKA 3-0 SHELISHELI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  TIMU ya taifa ya vijana ya Tanzaia chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Shelisheli katika mchezo wa kwanza wa raundi ya Kwanza kufuzu Fainali za U17 Afrika mwakani Madagascar. 
  Baada ya ushindi huo, Serengeti Boys itahitaji kwenda kulazimisha sare kwenye mchezo wa marudiano wiki ijayo Shelisheli ili kukata tiketi ya kwenda kukutana na Afrika Kusini.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Belay Tadesse Asserese, aliyesaidiwa na washika vibendera Tigle Giza Belachew na Kinfe Yilma Kinfe wote wa Ethiopia, hadi mapumziko, Tanzania walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
  Mfungaji wa bao la pili la Serengeti Boys, Ibrahim Abdallah Ali akikimbia kushangilia huku ameshika masikio yake, huku akifuatwa na mchezaji mwenzake, Kelvin Nashon Naftali (kulia). Mwingine ni beki wa Shelisheli, Stan Esther 

  Shaaban Zubeiry Ada alianza kuifungia timu ya kocha Bakari Nyundo Shime dakika ya 15 kwa shuti la umbali wa mita 19 kutoka upande wa kushoto wa Uwanja baada ya kupokea pasi ya Nickson Clement Kibabage.
  Shelisheli wakarudi nyuma ‘kupaki basi’ baada ya baada ya bao hilo ili kujizuia kuruhusu mabao zaidi ya ugenini na kuwapa wakati mgumu kidogo wenyeji.
  Hata hivyo, Ibrahim Abdallah Ali akafanikiwa kuifungia bao la pili dakika ya 22 Serengeti Boys inayonolewa pia na Mshauri wa Ufundi wa Shirikisho (TFF) kwa program za Vijana, Mdenmark Kim Poulsen.
  Ibra Ali alifunga bao hilo baada ya kuupitia mpira uliomponyoka kipa wa Shelisheli, Juninho Mathiot kufuatia shuti dhaifu la Kibabage, aliyekuwa anapanda mno kusaidia mashambulizi licha ya kucheza beki ya kushoto.
  Serengeti Boys ilipoteza nafasi mbili zaidi za kufunga baada ya kuwa inaongoza kwa mabao 2-0 kabla ya mchezo kwenda mapumziko.

  Beki wa Serengeti Boys, Nickson Clement Kibabage (kulia) akimtoka beki wa Shelisheli, Darren Dolley (kushoto)
  Mshambuliaji wa Serengeti Boys, Rashid Mohamed Chambo (kulia) akimtoka beki wa Shelisheli, Mathiew Bassot (kulia)

  Kiungo wa Serengeti Boys, Asad Ali Juma (kulia) akifumua shuti mbele ya kiungo wa Shelisheli, Jesus Joseph 

  Na kipindi cha pili, Serengeti Boys walifanikiwa kuunenepesha ushindi wao kwa bao la tatu lililofungwa kwa penalti na beki wa kati Ally Hussein Msengi dakika ya 62, baada ya beki wa Shelisheli, Stan Esther kuunawa mpira wa adhabu wa Asad Ali Juma katika ukuta.
  Serengeti Boys iliendelea kulisakama lango la wageni wao, lakini hawakufanikiwa kupata mabao zaidi.
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Ramadhan Kabwili, Israel Patrick Mwenda/Enrick Vitalis Nkosi dk73, Nickson Clement Kibabage, Dickson Jickson Job, Ally Hussein Msengi, Ally Hamisi Ng’azni, Kelvin Nashon Naftali/Cyprian Ben Mtesigwa dk46, Shaaban Zubeiry Ada, Ibrahim Abdallah Ali, Rashid Mohammed Chambo na Asad Ali Juma/Mohammed Rashid Abdallah dk85.
  Shelisheli; Juninho Mathiot, Gino Pleursuse, Mathiew Bassot/Tyjee Jeubort dk60, Stan Esther, Brandon Molle, Darren Dolley, Cuurtell Rose/Emmanuel Lesparanie dk89, Jesus Joseph, Hegled Havelock, Ryan Henrette na Brandon Tancustte.     
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SERENGETI BOYS YAITANDIKA 3-0 SHELISHELI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top