• HABARI MPYA

  Alhamisi, Juni 23, 2016

  BIN SLUM YAONGEZA MKATABA NA MBEYA CITY

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KAMPUNI ya Bin Slum Tyres Limited kupitia betri zake maarufu za RB, leo imeongeza Mkataba wa udhamini na klabu ya Mbeya City FC ya Mbeya.
  Zoezi hilo limefanyika mchana wa leo katika hafla maalum fupi iliyofanyika kwenye ofisi za Bin Slum Tyres Limited, Lumumba, Dar es Salaam.
  Akizungumza baada ya kukamilisha zoezi hilo, Naibu Mkurugenzi wa Bin Slum Tyres Limited, Mohammed Bin Slum alisema kwamba wameamua kuiongezea Mkataba klabu hiyo baada ya kuridhishwa na mwenendo wa timu hiyo.
  Mohammed, kiungo wa zamani wa Coastal Union ya Tanga amesema Mkataba mpya na utakuwa na thamani sawa na Mkataba wa awali.
  Naibu Mkurugenzi wa Bin Slum Tyres Limited, Mohammed Bin Slum (kushoto) akitiliana saini mikataba na Meya wa Manispaa ya Mbeya, David Polela Mwashilindi (kulia) leo mjini Dar es Salaam 

  “Tunayo furaha kuongeza Mkataba na Mbeya City baada ya ule wa awali kumalizika na tumefanya hivi baada ya kuvutiwa na mwenendo wao mzima,”amesema Bin Slum.
  Katika hafla hiyo, Mkurugenzi huyo pia aliwakabidhi vifaa vya michezo vya msimu mpya, vyenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 50 ikiwa ni pamoja na seti tatu za jezi. 
  Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Mbeya, David Polela Mwashilindi aliwashukuru Bin Slum kwa kuiteua Mbeya City kati ya timu nyingi za Tanzania na kusema wataendelea kuiwakilisha vyema kampuni hiyo.
  Katibu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe amewashukuru Bin Slum Tyres kwa kuendelea kuwadhamini na akaahidi watalipa fadhila kwa kutwaa taji msimu ujao.
  “Tutajitahidi msimu ujao tulete Kombe lolote hapa, ili kulipa fadhila kwa udhamini huu, kama si la Ligi Kuu basi Kombe la TFF, tutakuletea hapa,”alisema Kimbe kumuambia Bin Slum.
  Bin Slum Tyres Limited iliingia Mkataba na Mbeya City kwa mara ya kwanza mwaka 2014 ikiwapa dau la Sh. Milioni 360, yaani Sh. Milioni 180 kwa mwaka.
  Fedha hizo ni nje ya vifaa vya michezo wanavyopewa kila mwaka, ambavyo ni pamoja na seti tatu za jezi za kisasa kila msimu.
  Na mwaka jana Bin Slum Tyres Limited iliwakabidhi Mbeya City basi jipya kubwa la kisasa lenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 200.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BIN SLUM YAONGEZA MKATABA NA MBEYA CITY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top