• HABARI MPYA

  Jumatano, Juni 29, 2016

  HANS POPPE: YANGA WAMELITIA AIBU TAIFA KWA BUTUA BUTUA YAO

  Na Princes Asia, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema Yanga jana wamelitia aibu taifa kwa kucheza soka mbovu wakifungwa 1-0 na TP Mazembe ya DRC.
  Yanga jana imepoteza mechi ya pili mfululizo ya Kundi A, Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa 1-0, bao pekee Mereveille Boppe aliyemalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Chrtistian Luyindama dakika ya 74.
  Na baada ya kipigo cha hicho pili mfululizo ikitoka kufungwa 1-0 na wenyeji MO Bejaia 1-0 nchini Algeria, Hans Poppe amesema Yanga hawatafika mbali.
  Hans Poppe amesema Yanga jana wamelitia aibu taifa kwa kucheza soka mbovu

  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo Dar es Salaam, Hans Poppe amesema Yanga watamaliza mkiani wa kundi hilo na hatarajii kama watapata hata sare zaidi ya kufungwa mechi zote.  
  “Wamecheza mpira mbovu wa kubutua butua tu kama wanavyocheza Ligi ya hapa nyumbani, kwa mchezo ule hawafiki popote, wameitia aibu tu nchi yetu, tunaonekana wote hatujui mpira,”amesema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
  “Tena Mazembe hawakufunguka jana, walicheza kwa kuwategea wakapata bao lao moja na mpira wa adhabu kwa sababu wanajua kutumia nafasi zile. Sijafurahishwa na Yanga hata kidogo, wamelitia aibu taifa,”alisema.
  Yanga itahitimisha mechi zake za mzunguko wa kwanza za Kundi A kwa kucheza na Medeama ya Ghana Agosti 7 Uwanja wa Taifa pia na Hans Poppe amesema; “Hata wale wa Ghana wanakuja kujipigia tu, Yanga kelele tu na kubebwa, mpira hakuna,”.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HANS POPPE: YANGA WAMELITIA AIBU TAIFA KWA BUTUA BUTUA YAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top