• HABARI MPYA

    Wednesday, March 05, 2014

    SIMBA SC YAWAKANA MASHABIKI WAKE WALIOVUNJA VITI YANGA NA AL AHLY, YASEMA LABDA WA COASTAL...

    Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
    UONGOZI wa Simba umekanusha vikali mashabiki wake kuhusika na vurugu zilizotokea katika mpambano wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kati ya Yanga na Al Ahly uliochezwa mwishoni mwa wiki Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ulitawaliwa na vurugu kiasi kutoka kwa mashabiki kufuatia bao la Yanga lililofungwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambapo baadhi ya mashabiki waling’oa viti na kuanza kurushiana.
    Wenye jezi nyekundu mashabiki wa timu gani? Mashabiki wa Yanga SC kulia wakipambana kwa viti walivyong'oa uwanjani na mashabiki wa Simba SC wakati wa mchezo dhidi ya Al Ahly Jumamosi. Hata hivyo, uongozi wa Simba SC umewakana mashabiki wao na kusema ni wa Al Ahly au Coastal Union ya Tanga kwa sababu nayo inatumia jezi nyekundu.  

    Baadhi ya watu walidai kuwa vurugu hizo zilifanywa na mashabiki wa klabu za Simba na Yanga lakini hata hivyo uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi wamekanusha vikali taarifa hizo wakidai kuwa mashabiki wao hawawezi kufanya hivyo kutokana na kutokuwa na maslahi na mchezo husika.
    Ofisa Habari wa Simba, Asha Muhaji amesema leo katika taarifa yake kwamba, mashabiki wao hawawezi kufanya jambo hilo kwani mchezo huo ulikuwa ukiwahusu Yanga na Al Ahly na wala haukuwahusu kabisa Simba hivyo ni jambo la ajabu kuhusishwa kwa klabu yake katika tukio hilo.
    “Sisi tunaamini waliofanya vile ni mashabiki wa Al Ahly kwani ndio waliokuwa wapinzani wa Yanga siku hiyo, kwanza inashangaza Simba tunahusikaje katika mechi tusiyokuwa na maslahi nayo, pia ikumbukwe uongozi wa Simba siku zote umekuwa ukipinga vitendo vya uvunjifu wa amani zikiwemo vurugu, sasa mtu anaposema Simba imehusika mimi nadhani  wana agenda ya siri kutaka kuichafua klabu yetu,” alisema.
    Akizungumzia kigezo cha wahusika kuvaa jezi zenye rangi nyekundu inayotumiwa na klabu yake alisema, si kweli Simba ndiyo inayotumia jezi zenye rangi nyekundu pekee.
    “Ukiachilia mbali Al Ahly wenyewe, zipo pia timu nyingine hapa nyumbani zinazotumia rangi kama hiyo kama vile Coastal Union, Small Simba nk. ingawa simaanishi kama ndizo zilizohusika na tukio hilo hapana, nachotaka kusisitiza kuwa rangi si kigezo cha kumtuhumu mtu, ningependa Simba isihukumiwe kwa hilo”. Alisema.
    Asha alisema klabu yake ilishawahi kukatwa fedha zaidi ya Sh Milioni 25 kwa kosa kama hilo mwaka jana huku wahusika wakiwa hawana ushahidi wa kutosha hivyo amezitaka  mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na matukio kama hayo kabla ya kuamua kuziadhibu klabu kwa kigezo cha dhana tu.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAWAKANA MASHABIKI WAKE WALIOVUNJA VITI YANGA NA AL AHLY, YASEMA LABDA WA COASTAL... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top