• HABARI MPYA

  Jumamosi, Machi 22, 2014

  UMONY, AGGREY WAREJEA AZAM FC KUIVAA OLJORO KESHO CHAMAZI

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  MSHAMBULIAJI Mganda, Brian Umony anatarajiwa kurejea uwanjani kesho timu yake, Azam FC ikimenyana na JKT Oljoro katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Umony alitarajiwa kurejea uwanjani katikati ya wiki Azam ikimenyana na mabingwa watetezi, Yanga SC na kutoka sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lakini alijitonesha siku mbili kabla ya mchezo huo. 
  Rasta anarudi;Brian Umony anatarajiwa kurejea uwanjani kesho baada ya kukosa mechi mbili
  Aggrey Morris pia anatarajiwa katika mchezo wa kesho na JKT Oljoro

  Umony amekosa mechi mbili mfululizo zilizopita za Azam FC kutokana na maumivu ya kifundo cha mguu, lakini kesho kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog anaweza kumuanzisha.
  Beki Aggrey Morris aliyeshitua nyama katika mchezo na Coastal Union Chamazi, Azam FC ikishinda 4-0 hata akakosa mechi iliyopita na Yanga, naye kesho anatarajiwa kurejea uwanjani dhidi ya Oljoro.
  Azam FC ambayo itamkosa beki wake wa kulia Erasto Nyoni anayetumikia adhabu ya kadi mbili za njano alizopewa katika mechi moja na Yanga, itamkosa pia na beki Sammih Hajji Nuhu ambaye bado majeruhi sawa na viungo Ibrahim Mwaipopo, Farid Mussa na Joseph Kimwaga.
  Azam FC kesho itajaribu kujivuta mbele zaidi kileleni mwa ligi hiyo katika mbio za ubingwa itakapomenyana na Oljoro ikihitaji kujiongezea pointi kutoka 44 ilizonazo sasa baada ya mechi 20.
  Yanga SC yenye pointi 40 za mechi 19, leo inamenyana na Rhino Rangers Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora na ikishinda itaisogelea Azam kileleni. 

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: UMONY, AGGREY WAREJEA AZAM FC KUIVAA OLJORO KESHO CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top