• HABARI MPYA

  Jumapili, Machi 30, 2014

  YANGA SC CHALI MKWAKWANI, YAPIGWA 2-1 NA MGAMBO PUNGUFU

  Na Baby Akwitende, Tanga
  YANGA SC imekula ngwala katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Hadi mapumziko tayari Mgambo JKT walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na Fully Maganga dakika ya kwanza tu ya mchezo akimalizia pasi ya Bashiru Chanacha.
  Lilikuwa ni shuti la ghafla alilofumua mchezaji huyo mara tu baada ya kupata pasi, ambalo lilimkuta kipa Juma Kaseja akuiwa hajajiandaa kuokoa na kumpita kiulaini.
  Hawa Mgambo hawafai; Kocha wa Yanga SC, Hans van der Pluijm leo amefungwa 2-1 na Mgambo Tanga

  Mgambo ilipata pigo dakika ya 30 baada ya mchezaji wake, Mohamed Neto kutolewa nje kwa kadi mbili za njano, ya kwanza akikataa kukaguliwa na refa Alex Mahagi na ya pili kuzozana na refa huyo akipinga kusachiwa kama amebeba hirizi.
  Dakika ya 32 kipa wa Mgambo, Saleh Tendega aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na Tony Kavishe.
  Kipindi cha pili Yanga SC walirudi kwa nguvu na kufanikiwa kusawazisha bao kwa penalti dakika ya 52 kupitia kwa Nahodha wake, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, baada ya bi wa Mgambo kuunawa mpira katika eneo la hatari.
  Mgambo walicharuka baada ya bao hilo na kuanza kushambulia mfululizo langoni mwa Yanga na dakika ya 63 wakapata bao la ushindi.
  Bao hilo lilifungwa kwa penalti na Malimi Busungu baada ya yeye mwenyewe kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki wa Yanga SC, Kevin Yondan.      
  Matokeo hayo yanaifanya Azam iendelee kubaki kileleni kwa pointi zake 53 baada ya mechi 23, wakati Yanga SC inabaki na pointi zake 46 baada ya mechi 22.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Juma Kaseja, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva/Hamisi Kiiza dk77, Hassan Dilunga, Didier Kavumbangu, Mrisho Ngassa/Hussein Javu dk61 na Emmanuel Okwi. 
  Mgambo JKT; Saleh Tendega/Tony Kavishe dk32, Salim Mlima, Salim Gilla, Bashiru Chanacha, Bakari Mtama, Novatus Lukunga, Mohammed Samatta, Peter Mwalyanzi/Awadh Yassin dk88, Mohamed Neto, Fully Maganga na Malimi Busungu. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC CHALI MKWAKWANI, YAPIGWA 2-1 NA MGAMBO PUNGUFU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top