• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 21, 2014

  YANGA SC WAINGIA TABORA ‘USIKU USIKU’ KUSAKA POINTI TATU ZA KUFUFUA MATUMAINI YA UBINGWA

  Na Renatus Mahima, Tabora
  YANGA SC wamefika Tabora usiku wa jana tayari kwa mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Rhino Rangers, Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini humo baada ya safari ya tangu asubuhi.
  Yanga SC ambayo Jumatano ililazimishwa sare ya 1-1 na Azam FC iliyokuwa pungufu baada ya Erasto Nyoni kutolewa kwa kadi nyekundu, leo itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mwinyi jioni.
  Kikosi cha Yanga SC kilichotoa sare ya 1-1 na Azam FC juzi

  Timu hiyo inayofundishwa na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm inahitaji kushinda mchezo wa kesho ili kufufua matumaini ya kutetea ubingwa wake, sasa ikiwa inaachwa kwa pointi nne na Azam iliyo kileleni. Azam ina pointi 44 za mechi 20 na Yanga ina pointi 40 za mechi 19.
  Rhino Rangers inayoshika mkia kwenye Ligi Kuu inapambana kuepuka kushuka Daraja, hadi sasa ikiwa na pointi 13 baada ya mechi 21 na imebakiza mechi tano ambazo wanatakiwa washinde zote waangalie mustakabali wao. 
  Mechi nyingine za ligi hiyo kesho, Kagera Sugar wataikaribisha Prisons Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na keshokutwa katika Uwanja huo huo, Azam FC wataikaribisha JKT Oljoro, Simba SC watakuwa wenyeji wa Coastal Union Uwanja wa Taifa, Mgambo JKT wataikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Ashanti United Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WAINGIA TABORA ‘USIKU USIKU’ KUSAKA POINTI TATU ZA KUFUFUA MATUMAINI YA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top