• HABARI MPYA

  Jumapili, Machi 23, 2014

  TIMU ZA MISRI ZAENDELEA KUTAMBA AFRIKA, WADI DEGLA YAWAKALISHA DJOLIBA KOMBE LA SHIRIKISHO

  Na Salum Esry, Cairo 
  TIMU ya Wadi Degla imejiwekea matumaini ya kusonga mbele katika Kombe la Shirikisho Afrika kufuatia ushindi wa mabao 2-0 jana nyumbani dhidi ya Djoliba ya Mali mjini Cairo, Misri.
  Kiungo Mohamed Talaat alifunga bao la kwanza dakika ya 55 kabla ya beki wa Djoliba, Abdoulaye Traore kujifunga katika dakika za majeruhi, Wamisri hao wakijipatia mtaji mzuri kuelekea mechi ya marudiano mjini Bamako wikiendi ijayo.
  Mohamed Taalat akiifungia Wadi Degla jana Cairo

  Pasi ya kiungo Abdul Fattah Agah kwenda kwa Saladin ilinaswa na Bathily, ambaye alimpasia Talaat kuwafungia wenyeji bao la kwanza.
  Dakika tano baadaye, kipa mkongwe Essam El-Hadary aliokoa mchomo mkali wa Hamidu Sinayoko na kuwanusuru wenyeji kufungwa.
  Katika dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za kawaida, Agah alimimina krosi ikamkuta Saladin, lakini Mhabeshi huyo alipiga mpira dhaifu uliombabatiza Traore akajifunga. Katika mechi nyingine za Shirikisho jana, Etoile du Sahel ilishinda nyumbani Tunisia bao 1-0 dhidi ya SuperSport United ya Afrika Kusini, AS Kigali ya Rwanda ilishinda 1-0 nyumbani dhidi ya Difaa El Jadida na How Mine ya Zimbabwe ilishinda 2-1 nyumbani dhidi ya Bayelsa United ya Nigeria.
  Michuano hiyo itaendelea leo, Medeama ya Ghana ikiikaribisha Zesco United ya Zambia, CS Constantine ya Algeria ikiikaribisha ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Ismailia ya Misri ikiikaribisha Petro Atletico ya Angola na Warri Wolves ya Nigeria ikiikaribisha CA Bizertin ya Tunisia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TIMU ZA MISRI ZAENDELEA KUTAMBA AFRIKA, WADI DEGLA YAWAKALISHA DJOLIBA KOMBE LA SHIRIKISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top