• HABARI MPYA

    Wednesday, March 05, 2014

    WACHEZAJI YANGA SC WALALAMIKA KUPEWA POSHO KIDUCHU BAADA YA KUIFUNGA AL AHLY, WASEMA MORALI IMESHUKA KUELEKEA MCHEZO WA MARUDIANO

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    WACHEZAJI wa Yanga SC wamelalamika morali yao imeshuka kuelekea mchezo wa marudiano na Al Ahly ya Misri Jumapili hii mjini Cairo kuwania kutinga Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sababu wamepewa posho kiduchu baada ya mchezo wa kwanza Jumamosi walioshinda bao 1-0.
    Wakizungumza na BIN ZUBEIRY kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wachezaji hao walisema kwamba, mara baada ya mchezo wa Jumamosi viongozi waliwapelekea posho ya Sh. 100,000 kila mchezaji na kuahidi kurudi kuwaongezea, lakini hawajatokea hadi leo na hakuna salamu zozote.
    Morali imeshuka; Wachezaji wa Yanga SC wamelalamika kupewa posho kiduchu baada ya kuifunga Al Ahly 1-0 Jumamosi na wamesema morali yao imeshuka kuelekea mchezo wa marudiano Jumapili mjini Cairo

    “Hatufanyi hivi kwa nia mbaya tunataka wana Yanga wote wajue kitu ambacho viongozi wametufanyia baada ya kupigana na kufanya jambo la kihistoria Jumamosi,”alisema mmoja wa wachezaji hao.
    Mchezaji mwingine akasema kwamba wanaamini kitu walichokifanya ni kikubwa na cha kihistoria ambacho kimewafurahisha wana Yanga wengi, lakini hawasiti kuweka wazi wameingiwa kinyongo kwa posho kiduchu waliyopewa.
    “Afadhali fedha isingepatikana, lakini fedha imepatikana nyingi ya viingilio (sh. Milioni 448), halafu unawapa wachezaji laki laki, kweli jamani hiyo ni haki?,”alilalamika mchezaji mwingine.  
    Juhudi za kumpata Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga SC, Seif Ahmed ‘Magari’ hazikufanikiwa na baadhi ya viongozi wengine waliopigiwa akiwemo Ofisa Habari, Baraka Kizuguto hawakupatikana walipotafutwa. 
    Lakini juzi, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza mapato ‘yaliyogunwa’ kutokana na idadi ya watu kuwa wengi na viingilio vilikuwa vikubwa.   
    TFF ilisema mechi hiyo ya Yanga dhidi ya Al Ahly ambao ni mabingwa wa Afrika iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliingiza Sh. 448,414,000.
    Ilisema mapato hayo yametokana na watazamaji 50,202 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 7,000, sh. 13,000, sh. 25,000 na sh. 35,000.
    Ilisema mgawo wa mapato hayo ulikuwa; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 68,402,135.59, gharama za kuchapa tiketi ni sh. 10,343,219, waamuzi na kamishna sh. 14,665,930 na matangazo sh. 15,679,000.
    Uwanja sh. 50,898,557.31, gharama za mchezo sh. 33,932,371.54, mgawo wa  TFF na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) sh. 33,932,371.54 wakati Yanga ilipata mgawo wa sh. 220,560,415.01.
    Kwa mgawo wa posho ya Sh. 100,000 kwa kila mchezaji, maana yake Yanga haijatumia zaidi ya Sh. Milioni 3 kati ya Sh. Milioni 220 kuwapa hongera ya ushindi wa kihistoria wachezaji wake.
    Mkubwa mbona hupatikani? Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga SC, Seif Magari (katikati) hajapatikana kuzungumzia madai ya wachezaji

    Jumamosi ilikuwa mara ya kwanza Yanga SC inashinda dhidi ya timu kutoka Misri na Kaskazini mwa Afrika kwa ujumla- na kati ya timu za Kaskazini ambazo zimekuwa zikiinyanyasa Yanga SC, Al Ahly inaongoza zikiwa zimekutana mara saba na vigogo hao wa Misri wameshinda mechi nne na kutoa sare mbili na kufungwa moja Jumamosi.  
    ‘Bismillah’ Yanga inakutana kwa mara ya kwanza na Al Ahly na timu za Kaskazini kwa ujumla ilikuwa ni mwaka 1982 katika Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa na katika mchezo wa kwanza mjini Cairo, Waarabu hao walishinda 5-0 na marudiano Dar es Salaam timu hizo zikatoka sare ya 1-1. 
    Zikakutana tena mwaka 1988 katika Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa mchezo wa kwanza ukimalizika kwa sare ya bila kufungana Dar es Salaam wakati marudiano mjini Cairo, Yanga wakabebeshwa 4-0. 
    Kabla ya Jumamosil, mara ya mwisho Yanga kukutana na Ahly ilikuwa mwaka 2009 katika Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa pia na mchezo wa kwanza Cairo, wakafungwa 3-0 wakati marudiano Dar es Salaam wakafungwa pia 1-0.
    Kikosi cha Yanga SC kipo kambini hoteli ya Bahari Beach na kesho kinatarajiwa kuondoka nchini kwenda Cairo, Misri kwa ajili ya mchezo wa marudiano Jumapili, kujaribu kuitoa mashindanoni kwa mara ya kwanza kabisa timu ya Kaskazini mwa Afrika tangu ianze kukutana nazo 1982.
    Mapema kabla ya mechi ya kwanza na Waarabu hao, kulikuwa kuna habari kwamba uongozi umekusanya fedha Sh. Milioni 200 kwa ajili ya kuwapa motisha wachezaji wake washinde mechi hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WACHEZAJI YANGA SC WALALAMIKA KUPEWA POSHO KIDUCHU BAADA YA KUIFUNGA AL AHLY, WASEMA MORALI IMESHUKA KUELEKEA MCHEZO WA MARUDIANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top