• HABARI MPYA

  Jumatatu, Machi 24, 2014

  YANGA SC WAAMUA KUPUNGUZA GHARAMA ZA UENDESHAJI TIMU, KAMBI SASA JANGWANI, MAZOEZI KAUNDA

  Na Zaituni Kibwana, Dar es Salaam
  YANGA SC imeweka kambi makao makuu ya klabu yake, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wake wa Jumatano Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Prisons ya Mbeya.
  Yanga SC jioni hii inafanya mazoezi katika Uwanja wake wa Kaunda, kujiandaa na mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam keshokutwa na baada ya hapo wachezaji watapanda vyumbani kupumzika.
  Inaonekana Yanga SC imeamua kupunguza gharama za uendeshaji wa timu katika hatua za mwishoni za Ligi Kuu, baada ya kuwekeza fedha nyingi tangu Januari kwa maandalizi ya timu.
  Kikosi cha Yanga SC kipo kambini Jangwani

  Mapema Januari, Yanga SC ilikwenda kuweka kambi ya karibu wiki mbili Uturuki na iliporejea ikafikia katika hoteli ya Kiromo, Bagamoyo mkoani, Pwani na imekuwa ikitokea huko kwenda kwenye mechi zake zote za Ligi Kuu tangu hapo.
  Wakati wa maandalizi ya michezo miwili ya nyumbani na ugenini dhidi ya Al Ahly ya Misri Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga iliweka kambi katika hoteli ya Ledger Bahari Beach, iliyopo eneo la Kunduchi mjini Dar es Salaam.
  Hata hivyo, ilitolewa na mabingwa hao mara nane Afrika barani kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya jumla ya 1-1 baada ya kila timu kushinda 1-0 nyumbani kwake.
  Na katika Ligi Kuu Yanga inaelekea kupoteza ubingwa kutokana na kuzidiwa pointi nne na Azam FC wanaonoza ligi kwa pointi zao 44, ingawa wamecheza mechi moja zaidi.
  Baada ya Azam kushinda 1-0 dhidi ya JKT Oljoro jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam inaonekana Yanga wamekata tamaa na hawataki kuwekeza fedha zaidi kushindana na timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Bakhresa na famili yake zaidi ya kujiweka sawa kwa nafasi ya pili.
  Bingwa wa Ligi Kuu hucheza Ligi ya Mabingwa na mshindi wa pili hucheza Kombe la Shirikisho. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WAAMUA KUPUNGUZA GHARAMA ZA UENDESHAJI TIMU, KAMBI SASA JANGWANI, MAZOEZI KAUNDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top