• HABARI MPYA

  Jumapili, Machi 23, 2014

  ZAMALEK YALAZIMISHA SARE YA 0-0 NA NKANA ZAMBIA, ESPERANCE YAANZA NA SARE PIA UGENINI

  Na Mwandishi Wetu, Kitwe
  MATUMAINI ya Nkana FC ya Zambia kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika yamepungua baada ya jioni ya leo kulazimishwa sare ya bila kufungana nyumbani na Zamalek ya Misri katika mchezo wa kwanza wa 16 Bora mjini Kitwe.
  Mabingwa mara tano Afrika, Zamalek wamefurahia matokeo ya sare ya 0-0 kwenye Uwanja wa Nkana, wakiamini watamalizia vizuri mchezo wa marudiano mjini Cairo wiki ijayo na kusonga mbele.
  Kocha Ahmed Hassan 'Mido' amefanikiwa mpango wa kulazimisha sare ugenini Jumamosi mbele ya Nkana FC

  Hii inakuwa mara ya tatu mfululizo mechi kati ya Nkana na Zamalek kumalizika kwa sare Zambia na mechi zilizopita wababe wa Misri wamekuwa wakienda kushinda nyumbani kwao na kusonga mbele.
  Katika mchezo wa leo, Nkana walianza vizuri wakisukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa wapinzani wao, Zamalek.
  Nkana ilipata nafasi ya kwanza nzuri dakika ya tatu tu kupitia kwa mshambuliaji Simon Bwalya, ambaye alipiga kichwa na mpira kupaa juu ya lango kufuatia krosi ya winga Bruce Musakanya akiwa ndani ya eneo la hatari.
  Mshambuliaji Ronald Kampamba, pia alipata nafasi nzuri dakika ya 10 akashindwa kuitumia alipopiga mpira wa adhabu uliopaa juu ya lango.
  Kocha wa Zamalek, Ahmed Hassan ‘Mido’ alikuwa nyota hivi leo uwanjani kutokana na namna alivyoiongoza vyema timu yake akiwa benchi na kulazimisha sare ya ugenini.
  Mido alilundika wachezaji saba nyuma ya mpira kwa muda mrefu wa mchezo na kuvuruga mipango ya Kampamba na Bwalya katika safu ya ushambuliaji ya Nkana.
  Mshindi wa jumla baada ya mechi ya marudiano atasonga mbele hatua ya makundi, wakati atakayetolewa ataangukia kwenye mechi za kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwezi ujao.
  Katika mchezo mwingine leo, AS Real ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 nyumbani mjini Bamako, Mali na Esperance ya Tunisia.
  Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi kati ya TP Mazembe ya DRC na Sewe Sport mjini Abidjan, Horoya ya Guinea itaanzia nyumbani na CS Sfaxien ya Tunisia, sawa na ES Setif ya Algeria itakayoikaribisha Coton Sport ya Cameroon, AC Leopards ya Kongo itakayoikaribisha Al-Hilal ya Sudan na AS Vita ya DRC itaanzia nyumbani na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini Uwanja wa Tata Raphael mjini Kinshasa, wakati mechi zote za marudiano zitachezwa Jumamosi ya Machi 29, mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ZAMALEK YALAZIMISHA SARE YA 0-0 NA NKANA ZAMBIA, ESPERANCE YAANZA NA SARE PIA UGENINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top