• HABARI MPYA

  Jumapili, Machi 23, 2014

  AS VITA YAIFUMUA KAIZER CHIEFS 3-0 LIGI YA MABINGWA

  Na Mwandishi Wetu, Kinshasa 
  TIMU ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini imekiona cha moto, baada ya kufumuliwa mabao 3-0 jioni hii na wenyeji AS Vita kwenye Uwanja wa Tata Raphael mjini Kinshasa, DRC katika mchezo wa kwanza Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Hat-trick ya Firmin Ndombe Mubele ndiyo jioni hii imeifanya AS Vita ijisogeze karibu na hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, wakiiachia Chiefs mzigo wa kupanda mlima katika mchezo wa marudiano nyumbani kukipiku kipigo hicho.

  Pamoja na kufungwa, Chiefs itabidi wajilaumu wenyewe, kwani walipata nafasi nyingi za kufunga, lakini wakashindwa kuzitumia kutokana na umaliziaji mbovu.
  Mchezo mwingine ambao umekwishamalizika jioni ya leo, Leopards ya Kongo Brazaville imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 nyumbani na Al Hilal ya Sudan Uwanja wa Denis Sassou N'Guesso (Dolisie).
  Jana Nkana FC ya Zambia ililazimishwa sare ya bila kufungana nyumbani na Zamalek ya Misri mjini Kitwe na AS Real ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 nyumbani mjini Bamako, Mali na Esperance ya Tunisia.
  Mechi nyingine zinazotarajiwa kuchezwa leo ni kati ya TP Mazembe ya DRC na Sewe Sport mjini Abidjan, Horoya ya Guinea na CS Sfaxien ya Tunisia, ES Setif ya Algeria na Coton Sport ya Cameroon, wakati mechi zote za marudiano zitachezwa Jumamosi ya Machi 29, mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AS VITA YAIFUMUA KAIZER CHIEFS 3-0 LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top