• HABARI MPYA

  Jumapili, Machi 30, 2014

  R.I.P. AFRICA BAMBATAA, MUZIKI WA DANSI ULIKUPENDA, KUSAGA NA RUGE WALIKUPENDA ZAIDI

  MUONGO uliopita muziki wa dansi ulikuwa juu na wengi walivutiwa kuwekeza kwenye biashara ya bendi.
  Hiyo ilisaidia mno vijana wengi wenye vipaji kujitokeza na kutuondoa katika zama za bendi kongwe Msondo na Sikinde.
  Wanamuziki wengi wanaofanya vizuri hivi sasa, ni ambao waliibuka muongo uliopita na kuibukia katika bendi tofauti, zikiwemo za mikoani.
  Nazungumzia watu kama akina Khalid Chokora, Chaz Baba, Jose Mara, Kalala Junior na mdogo wake Toto Kalala na wengineo.

  Sababu muziki wa dansi ulikuwa juu, uliwavutia wawekezaji na vijana kujiingiza kwenye sanaa halisi ya uimbaji kwa kupigiwa ala papo kwa papo.
  Diamond Sound iliyokuwa inamilikiwa na Freddy Rwegasira ikiwa na maskani yake ukumbi wa Silent Inn pale Mwenge, na FM International ya Felician Mutta iliyokuwa na maskani yake ukumbi wa FM, zamani Lang’ata na baadaye ASET, pale Kinondoni ziliibuka mwishoni mwa miaka ya 1990 na kuteka hisia za wengi.
  Wakati huo hakukuwa na vituo vingi vya Redio na Televisheni, lakini wamiliki wa bendi hizo wote kutoka mkoa wa Kagera walijua kuvitumia vituo vichache vilivyokuwapo pamoja na magazeti kuzitangaza bendi zao na zikawa maarufu zaidi.
  Mtoto wa mjini wakati huo kama hujaingia FM au Silent Inn- huna cha kusimulia kwa wajanja. Kumbi hizo zilikuwa zinafurika mno siku za maonyesho yake mwishoni mwa wiki.
  Idadi kubwa ya wanamuziki wa bendi hizo walikuwa wanatokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na wakatambulisha staili ya kutumia wacheza shoo, kwa hiyo waliliteka sana soko.
  Mwishoni kabisa mwa miaka hiyo ya 1990, ikaibuka bendi nyingine iliyojulikana kama African Stars ambayo yenyewe iliundwa na wanamuziki wazawa watupu.
  Lakini wamiliki wake wakaamua kupambana kuifanya iweze kushindana na FM na Diamond na walianza kwa tabu sana wakifanya maonyesho ya kiingilio kinywaji katika ukumbi wa Mango Garden, pale Kinondoni.
  Kijana aliyekuwa anafanya muziki wa Bongo Fleva pale Sinza miaka ya 1990 akijulikana kwa jina la Ramadhani Masanja ‘Banza Stone’ alikuwa miongoni mwa waasisi wa bendi hiyo katika safu ya uimbaji pamoja na Luiza Nyoni na Jessica Charles.
  Banza akatambulisha mtindo wa Kutwanga na Kupepea na kuufanya kuwa rap moja nzuri sana iliyovutia na Luiza na Jessica wakaweza kuicheza vizuri inapopigwa-iliwapendeza sana watu.
  Rap ya Kutwanga na Kupepeta ikapata umaarufu zaidi iliporekodiwa katika wimbo Kisa cha Mpemba, uliotungwa na Adolph Mbinga.
  Wimbo huo ulipoanza kuchezwa redioni watu walianza kuuliza kuhusu hiyo bendi na idadi ya watu waliokuwa wanakwenda Mango siku African Stars inatumbuiza ikaongezeka hadi utaratibu wa kulipa viingilio ukaanzishwa.
  Watu walizidi kuongezeka Mango kwa sababu walikuwa wanatoka sehemu tofauti za jiji la Dar es Salaam- na kwa sababu hiyo, wamiliki wa bendi hiyo wakaongeza maonyesho ili kuwasogelea watu.
  Walifanikiwa mno, kila walipokwenda kupiga kumbi zilifurika na vyombo vya habari vikazidi kuitangaza bendi hiyo, nayo ikajiimarisha kwa kuajiri wanamuziki zaidi ndipo wakaibuka akina Mwinjuma Muumin na Ally Choky.
  Vituo vya Redio na Televisheni nchini vikaanzisha vipindi maalum vyenye wasaa mzuri kwa ajili ya nyimbo za bendi- na hapo ndipo bendi zikawa zinashindana kutoa nyimbo nzuri.
  Kwa kweli muziki wa dansi ulipaa juu mno, watu walisikia nyimbo wakazipenda wakapiga simu kwenye Redio kuzichagua, albamu zilipotoka wakanunua- na wakawa wanaenda kuzisikiliza na kuzicheza live ukumbini.
  Hadi wanamuziki wakaona inawezekana kumiliki bendi zao wenyewe wakipata sapoti ya vyombo vya habari na Mwinjuma Muumin akawa mwanamuziki wa kwanza kuanzisha bendi yake, Double M Sound ambayo iliteka hadhira kabla ya baada ya muda mfupi kusambaratika. 
  Banza Stone naye ambaye baadaye alihamia TOT alikouboresha mtindo wa Achimenengule na kuwa mpinzani mkubwa wa Twanga Pepeta, naye akatoka kwenda kuanzisha bendi yake na Ally Choki akafuatia.
  Hadi Mawaziri wa Serikali yetu nao wakawekeza kwenye bendi, ukiachilia mbali wafanyabiashara wakubwa. Ushindani ukaongezeka kuanzia baina ya bendi kwa bendi na wanamuziki kwa wanamuziki- ushabiki nao ukachukua nafasi yake hadi kwenye vyombo vya habari.
  Maonyesho yaliyokuwa yanafanyika ukumbi wa Diamond Jubilee yaliwavutia wengi sana na kwa ujumla mambo yalikuwa mazuri sana kwa wamiliki wa bendi zilizofanikiwa kupata umaarufu wakati huo.
  Lakini bahati mbaya sana, sijui akatokea mdudu gani, kipindi kilichokuwa kinaongoza kupiga nyimbo za bendi zetu, Africa Bambataa cha Redio Clouds kikafa.
  Hapo ndipo umaarufu wa muziki wa bendi ulipoanza kuporomoka nchini. Wakati huo Clouds ilikuwa inapendwa mno na karibu kila mtu alikuwa anasikiliza Redio hiyo, hivyo kuua Bambataa ilikuwa sawa na kuvunja daraja lililokuwa linaolowaunganisha wapenzi wa muziki na bendi.     
  Redio nyingine nazo zikafuata mkumbo na hatimaye vipindi vya nyimbo za bendi vikakauka, badala yake sasa nguvu zikaelekezwa kwenye Taarab.
  Hivi sasa, ikifika mida ya mchana Redio zote za Tanzania zinapiga Taarab, muziki ambao unapata wakati mzuri pia kwenye magazeti na Televisheni pia- jiulize kwa nini Jahazi na Mashauzi zisipendwe.
  Sasa hivi hata wamiliki wa kumbi za starehe, wanawaambia mapromota wakitaka kufanya biashara za uhakika, wachukue Jahazi au Mashauzi- ni kwa sababu nyimbo zao ni maarufu na zinachezwa na vituo vyote vya TV na Redio.
  Leo Joseph Kusaga au Ruge Mutahaba wanaweza kuibuka na hoja ya msingi ya kuua kipindi cha Bambataa- au hao wamiliki wa vituo vingine waliofuata mkumbo? Ni Redio yao, ni uamuzi wao lakini kitu kikishakuwa na mguso wa jamii lazima kidogo maamuzi yake yapitie tafakuri nzito.
  Muziki wa dansi unaweza kurudi juu hata kesho, iwapo vituo vya Redio na Televisheni vitarudisha programu maalum kwa ajili ya bendi zetu. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: R.I.P. AFRICA BAMBATAA, MUZIKI WA DANSI ULIKUPENDA, KUSAGA NA RUGE WALIKUPENDA ZAIDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top