• HABARI MPYA

    Wednesday, March 05, 2014

    LAKI MOJA MOJA ILIKUWA POSHO YA MAFUTA TU, MZIGO WA MAANA MTAPATA LEO USIKU, UONGOZI YANGA WAWAAMBIA WACHEZAJI WAKE

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    UONGOZI wa Yanga SC umesema kwamba Sh 100,000 walizopewa kila mchezaji baada ya mechi dhidi ya Al Ahly ya Misri Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zilikuwa ni posho za mafuta ya gari zao, lakini usiku wa leo watapelekewa posho nzuri baada ya ushindi wa 1-0 siku hiyo.
    Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Mussa Katabaro ameiambia BIN ZUBEIRY jioni hii kwamba, anashangazwa na madai ya wachezaji hao kwamba wamepewa posho kiduchu wakati ukweli ni kwamba walipewa fedha kwa ajili ya mafuta ya gari zao.
    Mlipewa posho za mafuta, mzigo wa maana mtapata leo usiku; Uongozi wa Yanga SC umewatuliza wachezaji wake kwamba posho ya ushindi dhidi ya Al Ahly watapata leo

    “Sisi tuna utaratibu wetu tuliojiwekea kwa ajili ya hatua hii na wachezaji wetu watafurahi sana baada ya mechi ya marudiano iwapo wataitoa Al Ahly, siku ile tuliwapa fedha kidogo kama posho ya mafuta ya gari zao, kwa sababu walipewa mapumziko ya siku mbili kabla ua kurudi kambini,”alisema Katabaro.
    Aidha, Katabaro alisema kwamba uongozi wa Yanga SC jioni ya leo utawapelekea posho nzuri wachezaji wake waliopo kambini hoteli ya Bahari Beach, wakati donge nono linawasubiri baada ya mchezo wa marudiano, wakifanikiwa kuwatoa mabingwa hao wa Afrika.
    Pamoja na hayo, habari zaidi kutoka ndani ya Yanga SC, zinasema kwamba wachezaji wote wa klabu hiyo, leo wamelipwa mishahara yao ya Februari- hivyo wataondoka kesho kwenda Misri wakiwa vizuri.
    Mchana wa leo, BIN ZUBEIRY iliwanukuu wachezaji wa Yanga SC wakilalamika morali yao imeshuka kuelekea mchezo wa marudiano na Al Ahly ya Misri Jumapili hii mjini Cairo kuwania kutinga Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sababu wamepewa posho kiduchu baada ya mchezo wa kwanza Jumamosi walioshinda bao 1-0.
    Wakizungumza na BIN ZUBEIRY kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wachezaji hao walisema kwamba, mara baada ya mchezo wa Jumamosi viongozi waliwapelekea posho ya Sh. 100,000 kila mchezaji na kuahidi kurudi kuwaongezea, lakini hawajatokea hadi leo na hakuna salamu zozote.
    “Hatufanyi hivi kwa nia mbaya tunataka wana Yanga wote wajue kitu ambacho viongozi wametufanyia baada ya kupigana na kufanya jambo la kihistoria Jumamosi,”alisema mmoja wa wachezaji hao.
    Mchezaji mwingine akasema kwamba wanaamini kitu walichokifanya ni kikubwa na cha kihistoria ambacho kimewafurahisha wana Yanga wengi, lakini hawasiti kuweka wazi wameingiwa kinyongo kwa posho kiduchu waliyopewa.
    “Afadhali fedha isingepatikana, lakini fedha imepatikana nyingi ya viingilio (sh. Milioni 448), halafu unawapa wachezaji laki laki, kweli jamani hiyo ni haki?,”alilalamika mchezaji mwingine.  
    Juhudi za kumpata Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga SC, Seif Ahmed ‘Magari’ hazikufanikiwa na baadhi ya viongozi wengine waliopigiwa akiwemo Ofisa Habari, Baraka Kizuguto hawakupatikana walipotafutwa. 
    Lakini juzi, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza mapato ‘yaliyogunwa’ kutokana na idadi ya watu kuwa wengi na viingilio vilikuwa vikubwa.   
    TFF ilisema mechi hiyo ya Yanga dhidi ya Al Ahly ambao ni mabingwa wa Afrika iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliingiza Sh. 448,414,000.
    Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuondoka kesho Dar es Salaam kwenda Cairo tayari kwa mchezo huo wa marudiano Jumapili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LAKI MOJA MOJA ILIKUWA POSHO YA MAFUTA TU, MZIGO WA MAANA MTAPATA LEO USIKU, UONGOZI YANGA WAWAAMBIA WACHEZAJI WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top