• HABARI MPYA

    Thursday, November 01, 2012

    STEWART AWASILI KUICHINJA COASTAL UNION CHAMAZI LEO

    Stewart alivyopokewa Uwanja wa Ndege jana. Picha kwa hisani ya straikamkali.blogspot.com

    Na Mahmoud Zubeiry
    LEO NI LEO kwenye Uwanja wa Chamazi, maarufu kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ambako timu mbili zinazopigana vikumbo katika nafasi ya tatu, wenyeji Azam FC watamenyana na Coastal Union ya Tanga katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Hiyo ni moja kati ya mechi tamu za Ligi Kuu, zisizozihusisha Simba na Yanga, kwani ukiondoa wababe hao wa soka Tanzania, kama kuna timu nyingine inayoweza kufikiriwa japo kushika nafasi ya pili kwenye ligi hiyo, ni kati ya hizo, Azam na Coastal.
    Azam imekuwa katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu kwa muda mrefu, kabla ya kushushwa hadi nafasi ya nne ndani ya siku mbili mwishoni mwa wiki na Coastal ndio ya tatu sasa, nyuma ya Yanga na Simba, zinazolinganana kwa pointi.
    Coastal inayofundishwa na kocha mtaalamu, lakini ‘simpo tu’, Ahmed Morocco itamenyana na Azam leo ambayo itaongozwa na Kali Ongala, anayekaimu Ukocha Mkuu, kufuatia kufukuzwa kwa Mserbia, Boris Bunjak Jumatatu.
    Baada ya kufukuzwa kwa Bunjak, Azam imekwishamrejesha kocha wake wa zamani, Muingereza Stewart Hall ambaye alitua jana usiku na leo atakuwapo Chamazi.
    Bunjak ameondoka Azam baada ya kuiongoza timu katika mechi 16, akifungwa nne tu, zote dhidi ya Simba ikiwemo ya juzi ya Ligi Kuu, waliyofungwa 3-1 na kutoa sare tatu.
    Bunjak mwenye leseni ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), alitua Azam, Agosti 7, mwaka huu akitokea FC Damac ya Saudia Arabia aliyoanza kuifundisha mwaka jana na kabla ya hapo alifundisha klabu kibao za kwao, zikiwemo FK Sloga Kraljevo, FK Javor Ivanjica, Crvena Zvezda Gnjilane, FK Radnicki Nis, FC Uralan Elista, FK Mladi Radnik, FK Crvena Zvezda Beograd, Al-Shaab, FK Hajduk Kula na Al-Nasr.
    Awali, Bunjak aliyezaliwa Novemba 17, mwaka 1954 ( miaka 57), alicheza soka katika klabu za FK Sloga (Kraljevo), FK Vozdovac (Beograd), FK Radnicki (Kragujevac), FK Olimpia (Ljubljana), FK Sumadija (Arandjelovac), FK Sloga (Kraljevo), FK Borac (Cacak) na FK Sloga (Kraljevo).
    Stewart alifukuzwa kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo, kumpanga Mrisho Khalfan Ngassa katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya Yanga.
    Mserbia huyo anakuwa kocha wa tano kufukuzwa Azam, ndani ya miaka minne tangu ianze kucheza Ligi Kuu, 2008 baada ya Stewart, Mbrazil Neider dos Santos, Sylvester Marsh na Itamar Amorin, Mbrazil mwingine.
    Lakini Stewart angalau aliacha kumbukumbu ya taji na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi Januari, kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili, kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la Urafiki na Kagame mwezi uliopita, mambo ambayo bila shaka yamemfanya afikiriwe tena.
    Stewart ana sifa ya kutokuwa mbinafsi na mwenye kuwaamini watu wa chini yake, kwa mfano namna ambavyo alikuwa akimpromoti Kali Ongala. Alimkuta Kali kama mchezaji, lakini kwa sababu ya umri kumtupa mkono, akashauriana naye awe Kocha Msaidizi na mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, akakubali.
    Chini ya Stewart, Kali alikuwa akiachiwa timu aiongoze ili kumjengea kujiamini zaidi na mwezi uliopita aliachiwa timu kwenye Kombe la Urafiki, akaifikisha fainali, ambako ilifungwa na Simba kwa penalti kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90. 
    Yote kwa tote, Chamazi leo kinachotarajiwa ni soka safi, ile ya burudani, isiyokuwa na presha kutokana na timu hizo kutokuwa na mashabiki wenye ugonjwa wa moyo kama wale wa Simba na Yanga.
    Wakati huo huo: Stewart Hall alitua jana usiku mjini Dar es Salaam na kusema anataka Azam ishinde kila mechi kuanzia sasa baada ya kurejea kazini.
    Hall amerejea katika klabu yake ya zamani ya Azam baada klabu aliyokuwa akiifundisha Sofapaka ya Kenya inayomilikiwa na tajiri kukiri kwamba haiwezi kupambana na kampuni kubwa ya Azam ambayo imeahidi kumpa mshahara mara mbili ya waliokuwa wakimlipa Wakenya hao.
    Mashabiki waliokuwa uwanjani hapo wakipuliza mavuvuzela na kupiga ngoma, waliimba nyimbo mbalimbali ukiwamo uliosema "Hall amerejea, homa na presha za Simba na Yanga ziko juu."
    Baada ya kutua kocha huyo, alivishwa mataji ya maua na viongozi wa Azam waliokuwapo kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kwa ajili ya kumpokea.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: STEWART AWASILI KUICHINJA COASTAL UNION CHAMAZI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top