• HABARI MPYA

  Alhamisi, Novemba 22, 2012

  SUNZU KUENDELEA KUOGELEA KWENYE FWEZA MSIMBAZI

  Feliux Sunzu akitibiwa

  Na Mahmoud Zubeiry
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu Jr. ataongezewa mkataba baada ya kumaliza mkataba wake wa awali mwishoni mwa msimu katika klabu ya bingwa Tanzania Bara, Simba SC.
  Kiongozi mmoja wa Simba ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba klabu hiyo imeridhika na huduma ya mchezaji huyo mrefu na inahitaji kuendelea naye.  
  Kumekuwa na mawazo tofauti ndani ya Simba SC kuhusu Sunzu, ambaye kwa sasa ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi Tanzania, Sh Milioni 5, kwamba hachezi kwa kiwango cha fedha anazolipwa.
  Lakini wengine wanaamini Sunzu anawajibika vizuri na anastahili kwa fedha anayolipwa. Pamoja na hayo, hali ya kiuchumi ndani ya klabu hiyo kwa sasa, inatia shaka kama itaweza kuurudia mkataba ule ule wa Sunzu.
  Hata hivyo, habari zaidi zinasema kwamba Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ ameamua kumaliza suala la Sunzu kwa kumsainisha mkataba mpya hivi karibuni.
  Baada ya kumaliza mkataba wa awali, Simba ili kuendelea kuishi na Sunzu, inakadiriwa kumpa fedha ya dau la usajili, ambalo kwa mwaka haliwezi kuwa chini ya dola za Kimarekani 15,000 (zaidi ya Sh. Milioni 20 za Tanzania) na kukubaliana kuhusu mshahara uwe ule ule au mpya.
  Kulingana zengwe lililotawala juu ya dola za Kimarekani 3,500 anazolipwa Sunzu kuna uwezekano Simba ikataka kuuteremsha mshahara huo, lakini habari zilizopatikana jana zimesema kwamba Sunzu ataendelea kulipwa mshahara ule ule katika mkataba wake mpya.
  Kumalizika kwa mkataba wa Sunzu ni mtihani mwingine kwa Simba, ambayo kwa sasa inakabiliwa na kasheshe la kuingia mkataba mpya na mshambuliaji wake Mganda, Emmanuel Okwi ambaye yuko vizuri kisoka na anatolewa macho na Azam na Yanga.
  Na suala la usajili linaonekana kuwa zito kwa wakati huu, kwa sababu Kamati ya Utendaji ya Simba SC wiki hii imevunja Kamati zote ndogondogo, ikiwemo Kamati ya Usajili, iliyokuwa chini ya Mwenyekiti Zacharia Hans Poppe.   
  Hata hivyo, inadaiwa vibopa wa Kamati ya Usajili, akiwemo Hans Poppe watarejeshewa majukumu hayo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: SUNZU KUENDELEA KUOGELEA KWENYE FWEZA MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top