• HABARI MPYA

  Jumanne, Novemba 27, 2012

  NIYONZIMA ATAMANI KUBAKI YANGA, LAKINI...


  Haruna Niyonzima
  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
  KIUNGO wa Yanga, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima amesema kwamba iwapo Yanga watakubali ofa ya klabu ya El Merreikh ya Sudan, atakuwa radhi kuondoka klabu hiyo na kwenda kuanza maisha mapya Khartoum.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini hapa, Nahodha huyo wa Rwanda katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge alisema kwamba anaipenda sana Yanga lakini soka kwa sababu ni kazi yake, anaangalia maslahi pia.
  “Mimi walinifuata Merreikh, nikawaambia nina mkataba na Yanga, wawasiliane na Yanga. Kama Yanga watakubali, mimi nitaangalia maslahi tu, Merreikh wakinipa maslahi mazuri kuliko nayopata Yanga sitakuwa na tatizo,”.
  “Lakini kwanza, Yanga wao wenyewe wakubali kuniuza, wakikubali mimi sina tatizo, nawaheshimu sana Yanga wamenilea vizuri kwa kipindi chote nilichokuwa nao na ndiyo maana uwezo wangu haujayumba,”alisema Niyonzima.
  Lakini Haruna alisema ana ofa pia ya kwenda kucheza Ubelgiji, ingawa alisema hiyo ipo nusu kwa nusu tofauti na ya Merreikh ambao wameonyesha nia ya moja kwa moja ya kumuhitaji.
  “Kucheza Ulaya ni kitu ambacho kila mchezaji wa Afrika anakitaka, kama Mungu atapenda niondokee Yanga kwenda Ulaya, nitafurahi, na kama kuondokea Sudan, yote sawa, au nitamalizia soka yangu Afrika, yote sawa pia,”alisema.
  Niyonzima ni kati ya wachezaji wa Yanga wanaong’ara katika CECAFA Tusker Challenge, wengine wakiwa ni Hamisi Kiiza wa Uganda, Frank Domayo wa Tanzania Bara na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Zanzibar.   
  Niyonzima aliyesajiliwa Yanga mwaka jana kutoka APR ya nyumbani kwao, Rwanda jana aliiongoza nchi yake, kuifunga mabao 2-0 Malawi katika mchezo wa Kundi C, akiifungia Amavubi bao la pili kipindi cha pili, baada ya Jean Baptiste Mugiraneza kufunga la kwanza kipindi cha kwanza. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: NIYONZIMA ATAMANI KUBAKI YANGA, LAKINI... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top