• HABARI MPYA

    Wednesday, November 28, 2012

    SITAKI KUAMINI AHADI HIZI NI DANGANYA TOTO KUELEKEA MKUTANO MKUU YANGA


    KLABU ya Yanga, imetangaza kuwa na ziara ya nchini Uturuki kwa wiki mbili, kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, pamoja na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwakani.
    Na Mahmoud
    Bin Zubeiry
    Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb alisema mapema wiki hii, kwamba ziara hiyo itakuwa kati ya Desemba na  Februari 25, mwakani.
    Alisema pendekezo la kambi hiyo lilitolewa na kocha mkuu wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts ambaye ana uzoefu na nchi hiyo ambayo ina vitu vinavyostahili kwa ajili ya timu kuweka kambi.
    Alisema ikiwa huko timu hiyo inatarajiwa kucheza mechi mbili za kitrafiki na timu zitakazotajwa baadaye.
    Ahadi ya ziara ya Ulaya, inakuja siku chache tu, baada ya ahadi nyingine nzito zaidi kutolewa na uongozi wa klabu hiyo, ujenzi wa Uwanja mpya wa kisasa wa klabu hiyo, utakaokuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki kati ya 30,000 na 40,000.
    Ahadi zote hizi, zinakuja wakati klabu hiyo ikielekea katika Mkutano wake Mkuu wa kwanza wa mwaka, tangu kuingia madarakani kwa uongozi mpya chini ya Mwenyekiti, Alhaj Yussuf Mehboob Manji Julai 14, mwaka huu.
    Tayari Yanga wametangaza Mkutano Mkuu wa klabu hiyo utafanyika Desemba 8, mwaka huu katika ukumbi wa Dar Live, Mbagala, Dar es Salaam.
    Nianze tu kwa kusema, mimi ni miongoni mwa watu ambao wana imani kubwa na uongozi wa sasa wa Yanga chini ya Mwenyekiti Manji na ninaamini juu ya mikakati na ahadi zao.
    Lakini siku zote, watu wanapoingia katika uongozi wa soka nchini, mara nyingi huwa wanabadilika na kufuata mkumbo wa ubabaishaji. Sina shaka na viongozi wa Yanga juu ya hilo, lakini nataka kuendelea kuwapa tahadhari.
    Wiki iliyopita, nilizungumzia ahadi ya Manji kujenga Uwanja, nikasema Juni mwakani ambayo Mwenyekiti huyo ameahidi ujenzi utaanza, itafika tu kwa sababu siku hazigandi.
    Manji alisaini makubaliano ya awali na Kampuni ya Beijing Constructions Engineering Group iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Kaunda, unaomilikiwa na klabu hiyo.
    Manji alisaini makubaliano hayo na Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo, David Zhang, mbele ya Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam.
    Katika makubaliano hayo, ilielezwa ujenzi huo wa Uwanja utakaokuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 hadi 40,000 utaanza rasmi Juni mwakani.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa kusaini makubaliano hayo juzi mchana, Alhaj Manji alisema kwamba wanafurahi kuanza safari ya ujenzi wa Uwanja wao na anaamini huo ni mwanzo wa mzuri wa mipango yao ya kuifanya Yanga ijitegemee kiuchumi.
    Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Beijing Constructions Engineering Group alisema wanafurahia kufikia makubaliano ya awali ya ujenzi wa uwanja na klabu ya Yanga.
    Alisema wao ndio walijenga Uwanja wa Taifa na viwango vya ujenzi vya uwanja huo vilisifiwa na timu ya taifa ya Brazil iliyokuja kucheza mechi ya kirafiki na Tanzania mwaka 2010 ikiwa njiani kuelekea Afrika Kusini ambako fainali za kombe la Dunia zilifanyika.
    Nilikumbusha kwamba, Manji si Mwenyekiti wa kwanza wa Yanga kutoa ahadi ya kujenga Uwanja wa Kaunda na wakati juzi mkandarasi alifanya vipimo, nataka niwakumbushe tu wasomaji wangu, wakati Tarimba Abbas, Francis Kifukwe wakiwa viongozi wakuu wa klabu hiyo, walikwenda wakandarasi kupima Jangwani.
    Huo ni wakati ambao haijafikiriwa kama iko siku itatokea timu inaitwa Azam FC na leo klabu hiyo ina miaka sita, lakini Uwanja wa Kaunda upo kama alivyouacha marehemu Tarbu Mangara, tena umezidi kuchakaa kwa kukosa japo matunzo tu.
    Azam FC leo ina Uwanja wa maana na akademi, ambayo hadi Mwanasoka Bora wa zamani Afrika, Abedi Ayew Pele alipozuru nchini aliusifia.
    Nina kila sababu ya kumuamini Manji, kwa sababu kila ukiitazama Yanga ya leo, bila ya yeye sijui ingekuwaje.
    Manji aliingia Yanga mwaka 2006 baada ya jitihada zilizofanywa na wanachama wa klabu hiyo akina Theonist Rutashoborwa (sasa marehemu), Mzee wa Mpunga, Mawakili Lugaziya na Matunda na baadhi ya Waandishi wa Habari za michezo wenye mapenzi na klabu hiyo, kuanzisha harambee ya Saidia Yanga, kufuatia hali mbaya ya kiuchumi kukithiri ndani ya klabu hiyo, chini ya uongozi wa Francis Kifukwe.
    Katika kutafuta misaada ya kuibeba timu wakati huo ipo kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame ndipo wakampata Manji naye kwa mapenzi yake, akasema; “Nitaubeba mzigo wote”, na kweli hadi leo, amekuwa akiilea Yanga tangu kama mfadhili hadi sasa Mwenyekiti.
    Hadi sasa, Manji ameingia kwenye historia Yanga kama miongoni mwa watu muhimu kuwahi kutokea kwenye klabu hiyo, bila hata ya ahadi ya Uwanja na Ulaya.
    Kihistoria mara nyingi, inapokaribia mikutano ya wanachama, viongozi waliotangulia Yanga walikuwa wakitoa ahadi nzuri tamu, ili kuifanya mikutano iwe miepesi.
    Na hiyo ni desturi ambayo wanayo hata wapinzani wao wa jadi, Simba SC haswa katika kipindi hiki, ambacho wanaongozwa na Mwenyekiti ‘mjanja mjanja’ Alhaj Ismail Aden Rage.
    Narudia kusema, bado siamini kama uongozi wa Yanga chini ya Manji, utakuwa kama tawala zilizopita, zilizoiendesha klabu kisanii.
    Nina imani na Manji na safu yake nzima ya uongozi kwamba ni watu ambao wana mikakati waliodhamiria kuitekeleza ili kuleta mageuzi ndani ya Yanga. Sitaki kuamini kama ahadi hizi ni danganyo toto ya mkutano Mkuu! Wasalam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SITAKI KUAMINI AHADI HIZI NI DANGANYA TOTO KUELEKEA MKUTANO MKUU YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top