• HABARI MPYA

  Ijumaa, Novemba 30, 2012

  NIMEWALETEENI WANYELA, MSIJISIFU SANA, ASEMA KOCHA SUDAN

  Mubarak Suleiman

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
  KOCHA wa Sudan, Mubarak Suleiman amesema kwamba hawakuja na kikosi chao kamambe katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kutokana na wachezaji wao chaguo la awali kuwa na klabu zao, El Merreikh, Al Ahly Shandy na El Hilal kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini hapa, Suleiman alisema kwamba wachezaji aliokuja nao wanatoka klabu nyingine ndogo za nchini mwao na ndiyo maana timu yao haina makali yake yaliyozoeleka.
  “Tumekuja kushiriki ili kuwapa uzoefu wachezaji wengine, hatukuja na timu yetu ya kwanza kwa sababu wachezaji wote wapo na timu zao kwenye Kombe la Shirikisho,”alisema kocha huyo.
  Hata hivyo, Suleiman alisema kwamba wamekuja hapa kushindana na watajitahidi kadiri ya uwezo wao kupata matokeo mazuri.
  “Wachezaji hawa wageni wa mashindano makubwa, lakini taratibu watapata uzoefu na ninaamini katika mechi zijazo watafanya vizuri na tunaweza kufika mbali,”alisema.
  Sudan katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi B ilifungwa mabao 2-0 na Tanzania Bara wakati mchezo wa pili, ilishinda kwa mbinde 1-0 dhidi ya Somalia na kesho itakamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na Burundi.
  Hadi sasa uwezekano wa Sudan kutinga Robo Fainali, zaidi ni kama mmoja wa washindi wa tatu bora- kwani kesho itamenyana na Burundi, ambayo hadi sasa unaweza kusema ndio timu iliyoonyesha mchezo mzuri zaidi kwenye mashindano haya, ikiwa inaongoza Kundi B.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: NIMEWALETEENI WANYELA, MSIJISIFU SANA, ASEMA KOCHA SUDAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top