• HABARI MPYA

    Sunday, November 25, 2012

    KOCHA KENYA ALILIA KITASA CHA AZAM


    Shikanda
    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    KOCHA wa muda wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, James Nandwa amesikitika kumkosa beki wa Azam FC ya Tanzania, Ibrahim Shikanda katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, Tusker Challenge zinazoendelea mjini hapa.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY katika mahojiano maalum mjini hapa jana, Nandwa anayemshikia timu hiyo kwa muda Mfaransa Henri Michel, alisema kwamba alimuita Shikanda katika kikosi chake cha Tusker Challenge, lakini akashindwa kuja kwa sababu ni majeruhi.
    “Nilimuita Shikanda, lakini akasema yeye ni mgonjwa hawezi kuja, kwa kweli kwangu na kwa benchi zima la ufundi tumesikitika kumkosa beki mzuri kama Yule, ambaye anafanya vizuri hadi katika klabu yake,”alisema Nandwa.
    Hata hivyo, kocha huyo alisema kwamba anakubaliana na matokeo na ataendelea na wachezaji alionao kuhakikisha kwamba anarejea na Kombe Kenya.
    “Michuano ni migumu, hasa kundi letu, kama unavyoona tumefungwa na Uganda, lakini bahati haikuwa yetu. Tulitengeneza nafasi nyingi tukashindwa kuzitumia, wenzetu wametumia nafasi waliyopata.
    Na ugumu zaidi upo kwenye kundi. Hakuna timu dhaifu. Kuna Ethiopia ambao wamefuzu kucheza Fainali za AFCON (Mataifa ya Afrika). Sudan Kusini umewaona wameisumbua Ethiopia, hili ni kundi gumu sana,”alisema Nandwa.
    Hata hivyo, amesema watapambana kushinda mechi zao zote zilizosalia ili watinge Robo Fainali.    
    Kenya jana wameanza vibaya CECAFA Tusker Challenge baada ya kuchapwa na Uganda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mandela, uliopo Namboole, Kampala, Uganda.
    Mbaya wao jana alikuwa ni mshambuliaji wa Saigon Xuan Thanh ya Vietnam, Geoffrey Kizito aliyefunga bao hilo pekee la ushindi dakika ya 74, akiunganisha krosi ya Iguma Dennis.
    Kwa ushindi huo, Korongo wa Kampala anafungana na Ethiopia kuongoza Kundi A, kwa pointi zake tatu kila timu. 
    Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na timu zote zilishambuliana kwa zamu.
    Kenya walianza kwa kasi kwa dakika tano wakicheza soka iliyowasisimua mashabiki wake wachache waliokuwapo uwanjani, lakini Uganda wakazinduka nao na kuanza kuwapa raha mashabiki wao kwa soka safi.
    Mchezo uliendelea kuwa hivyo kwa timu hizo kushambuliana kwa zamu, kila upande wakicheza kwa kujiamini.
    Lakini sifa ziende kwa safu zote mbili za ulinzi kutokana na kucheza kwa umakini wa hali ya juu.
    Kipindi cha pili timu hizo ziliporejea uwanjani, zililazimika kusimama kwa takriban dakika saba baada ya taa za uwanjani kuzimika na baada ya mafundi kutatua tatizo hilo, ndipo kabumbu likaanza tena.  
    Michuno hiyo itaendelea kesho kwa mechi mbili, Burundi na Somalia saa 10:00 jioni na baadaye Tanzania Bara na Sudan saa 12:00 jioni.
    Uganda; Abel Dhaira/Hamza Muwonge, Iguma Dennis, Godfrey Walusimbi,Henry kalungi, Isaac isinde, Hassan Wasswa, Geoffrey Kizito, Moses Oloya, Emmanuel Okwi, Hamisi Kiiza na Brian Umony.
    Kenya; Duncan Ochieng, Anthony Kimani, Abdallah Juma, Jockins Atudo, David Owino, David Ochieng, Lama Salim Mohamed, Bernard Wanyama, Humphrey Mieno, Anthony ‘Muki’ Kimani/Enock Obiero na Clifton Miheso/Paul Were.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KOCHA KENYA ALILIA KITASA CHA AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top