• HABARI MPYA

    Wednesday, November 21, 2012

    BARTHEZ ALIVYOMNUSURU YAW BERKO KUTUPIWA VIRAGO YANGA

    Ally Mustafa 'Barthez'

    Na Mahmoud Zubeiry
    WASIWASI kwamba Ally Mustafa ‘Barthez’ akibaki bila kipa mshindani ndani ya Yanga atabweteka, ndio umemnusuru kipa Mghana, Yaw Berko kutemwa Yanga.
    Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani ya Yanga, zimesema kwamba, Yanga ilifikiria kumtema Berko, lakini kwa uzoefu wao juu ya tabia za wachezaji wa Kitanzania, wameamua kuachana na wazo hilo.
    “Unaweza kusema umuache Berko, halafu yule Barthez akijiona yuko peke yake, akaanza kutuzingua, Berko mwenyewe amebadilika mno hivi sasa na yuko tayari kucheza wakati wowote,”alisema kiongozi mmoja ‘mzito’ wa Yanga.
    Berko ambaye mkataba wake unamalizika Mei mwakani, ataendelea kuitumikia klabu hiyo hadi mwisho wa mkataba huo na akifanya vizuri ataongezewa mkataba mwishoni mwa msimu.
    Kipa huyo anayelipwa mshahara wa Sh. Milioni 1.5 kwa mwezi, amerudishwa benchi siku za karibuni baada ya kufululiza kufungwa mabao rahisi, jambo ambalo lilimkera kocha Mholanzi, Ernie Brandts.
    Kwa sababu hiyo, vyombo vya habari vikaanza kubashiri kwamba ataachwa mwezi ujao kwa sababu pia, tayari klabu hiyo imesajili mchezaji mwingine wa kigeni, Kabange Twite kutoka APR ya Rwanda.
    Kanuni za Usajili za Ligi Kuu zinataka wachezaji watano tu wa kigeni kwa kila klabu, na Yanga tayari inao Yaw Berko, Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima kutoka Rwanda, Hamisi Kiiza kutoka Uganda na Didier Kavumbangu kutoka Burundi.
    Lakini habari zaidi zinasema Kabange atachukua nafasi moja kati ya mbili zinazotarajiwa kuachwa na wachezaji wawili wa klabu hiyo, ambao watauzwa hivi karibuni, Niyonzima na Kavumbangu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: BARTHEZ ALIVYOMNUSURU YAW BERKO KUTUPIWA VIRAGO YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top