• HABARI MPYA

  Ijumaa, Novemba 23, 2012

  TRA YAFUNGA AKAUNTI ZA TFF


  Na Prince Akbar
  MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara huko mashakani kufanyika baada ya Mapato ya Taifa(TRA) kuzifunga akaunti za udhamini wa ligi hiyo.
  TRA ilizifunga akaunti za TFF ikiwemo ya udhamini wa ligi hiyo ikiwa ni sehemu ya kulishinikiza Shirikisho la Soka nchini(TFF) kulipa makato ya kodi kwenye mishahara ya timu ya taifa(Taifa Stars) tokea kipindi cha kocha Marcio Maximo.
  Akizungumza na waandishi wa habari jana Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini(TFF) Sunday Kayuni alisema mishahara ya makocha wa Taifa Stars tangia kocha Marcio Maximo ilikuwa haikatwi kodi na hivyo kufanya gharama wanazodaiwa na mamlaka ya Mapato kufikia shilingi milioni 157,407.968.00.
  Alisema wamekuwa wakipata taarifa ya mara kwa mara toka TRA ikiwakumbusha juu ya makato hao na wao kuwajibu kuwa hawahusiki kwenye malipo ya mishahara ya makocha hao kwani ni waajiriwa wa Serikali.
  Kayuni alisema hata hivyo kwa kuwa wao ndio walezi wa makocha hao TRA imeamua kuzifunga akaunti zao ikiwemo ya udhamini wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara ambayo ina zaidi ya shilingi milioni 300.
  Alisema kutokana na hali hiyo walifanya mazungumzo ya mara kwa mara na TRA bila ya mafanikio na kuamua kuunda kamati itayoshirikisha Kamati ya Ligi ikishirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo kwa ajili ya kufanya mazungumzo na mamlaka hiyo ya mapato nchini.
  “Tunaona labda tukiunganisha nguvu zetu labda wenzetu wa TRA wanaweza kutusikiliza, hivyo Kamati tutakayounda kwa kushirikiana na wizara itakwenda kujaribu kufanya tena mazungumzo na TRA.”alisema Kayuni.
  Kwenye Mkutano huo na waandishi wa habari Kayuni aliambatana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi Kuu Saidi Mohamedi na Mkurugenzi Mkuu wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara Silas Mwakibinga, ambao wote walionyesha umuhimu wa kuunganisha nguvu zao kuishawishi TRA.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: TRA YAFUNGA AKAUNTI ZA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top