• HABARI MPYA

    Monday, November 26, 2012

    KOCHA BURUNDI AMTEMA KAVUMBANGU KIKOSI CHA TUSKER CHALLENGE 2012

    Kocha wa Burundi, Lotfy Mohamed

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    KOCHA wa timu ya soka ya taifa ya Burundi, Int’hamba Murugamba, Mmisri Lotfy Mohamed amesema kwamba amemtema kwenye kikosi chake mshambuliaji wa Yanga SC ya Dar es Salaam, Didier Kavumbangu kwa sababu hamuhitaji kwenye mipango yake ya sasa.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini hapa, Mohamed alisema kwamba amekuja na kikosi cha wachezaji ambao wanacheza Ligi ya Burundi pekee na hajachukua mchezaji hata mmoja anayecheza nje.
    Amesema sababu ya kufanya hivyo ni kuanza kuwaandaa wachezaji wa kucheza michuano ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za CHAN, ambazo huhusisha nyota wanaocheza ligi za nyumbani kwao pekee.
    “Siyo Kavumbangu tu, kuna wachezaji wengine wazuri tu wanaocheza hadi Ulaya, lakini sikuwachukua, kwa sababu siwahitaji katika mipango yangu ya sasa, bado ni wachezaji wa timu ya taifa na naheshimu uwezo wao,”alisema Mohamed.
    Kavumbangu alisajiliwa Agosti mwaka huu Yanga akitokea Atletico ya Burundi, baada ya kung’ara kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Komnbe la Kagame.
    Bila Kavumbangu na mastaa wengine wa nje, ikiongozwa na mkongwe Suleiman Ndikumana anayechezea Inter Stars ya nyumbani kwao kwa sasa, Burundi iliichapa Somalia mabao 5-1 jana katika mchezo wa Kundi B wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge.
    Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala, mabao ya Burundi yalifungwa na Chris Nduwarugira dakika ya 35 na 88, Yussuf Ndikumana dakika ya 41 na Suleiman Ndikumana dakika ya 84 na 90, wakati la Somalia lilifungwa na Mohamed Jabril kwa penalti dakika ya 55. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KOCHA BURUNDI AMTEMA KAVUMBANGU KIKOSI CHA TUSKER CHALLENGE 2012 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top