• HABARI MPYA

  Jumanne, Novemba 27, 2012

  POULSEN ASEMA VIJANA WANAKOMAA, MATUMAINI YA NDOO YAPO


  Kilimanjaro Stars
  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
  KOCHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Mdenmark Kim Poulsen amesema kwamba uwezo wa timu yake unazidi kukua siku hadi siku na sasa ana matumaini ya kufanya vizuri zaidi katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA, Tusker Challenge.
  “Tuliwafunga Kenya, tumewafunga Sudan, timu zote nzuri, Sudan wapo juu yetu kiuwezo katika viwango vya FIFA. Kwangu siangalii sana viwango vya FIFA, mpira ni pale unapokuwa uwanjani,”alisema Poulsen.
  Akilizungumzia kundi lake, B lenye timu za Sudan, Somalia na Burundi, alisema ni gumu na wanatakiwa kupambana ili kufika mbali.
  Lakini Poulsen amesema bado anawahitaji mno washambuliaji Mbwana Ally Samatta na Thomas Emanuel Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) , ambao wamezuiwa na klabu yao.
  Kim alisema jitihada za kuwaomba Mazembe wawaruhusu wachezaji hao zinaendelea.
  “Sijui itakuwaje wasipokuja, itanibidi tu niwatumie wachezaji hawa hawa waliopo, najua nina mshambuliaji mmoja, lakini nitawatumia hawa hawa waliopo, Simon Msuva anaweza akawa mshambuliaji, nitafanyeje,”.
  “Siwezi kuita mchezaji mwingine kutoka nyumbani kwa sasa, kwa sababu mtu lazima umuone uwezo wake, huwezi kumuita tu, kwa hivyo naomba Mungu tu Samatta na Ulimwengu waje,”alisema Kim.
  Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, jana ilianza vema kampeni zake za kuwania Kombe la Challenge, baada ya kuichapa mabao 2-0 Sudan juzi kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala, Uganda. 
  Ushindi huo, unaiweka Stars katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi B, nyuma ya Burundi inayoongoza kwa wastani wa mabao.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: POULSEN ASEMA VIJANA WANAKOMAA, MATUMAINI YA NDOO YAPO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top