• HABARI MPYA

  Ijumaa, Novemba 30, 2012

  STARS NA SOMALI KUCHEZA UWANJA KAMA WA LEADERS TU DAR

  Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye akizungumza na Waandishi wa Habari leo katika ofisi za FUFA, Kampala, kulia kwake ni Ofisa Habari wa FUFA, Rodgers Mulindwa na Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya FUFA, Moses Magogo.

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
  BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limezihamisha mechi za mwisho za Kundi B na C Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kutoka Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa hadi Uwanja wa Lugogo, uliopo katikati ya mji ambao ni mfano wa viwanja kama TCC Chang’ombe au Leaders Club pale Dar es Salaam.
  Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye amewaambia Waandishi wa Habari leo katika Mkutano uliofanyika ofisi za Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), kwamba sababu ya kuzihamishia mechi hizo huko ni hali mbaya ya Uwanja wa Namboole kwa sasa kutokana na mvua.
  “Tunataka Uwanja wa Namboole upumzike, kwa hivyo mechi zote za mwisho za Kundi B na C zitachezwa Lugogo,”alisema Musonye, raia wa Kenya.
  Aidha, Musonye alisema kwamba mechi ya Robo Fainali itakayoihusisha Uganda, itachezwa Jumanne kwenye Namboole, wakati mechi nyingine za hatua hiyo zitachezwa Lugogo.
  Hata huvyo, Musonye amesitikitishwa na mahudhurio ya watu kwenye mechi za mashindano ya mwaka huu kuwa madogo na kuvitaka vyombo vya habari kuhamasisha zaidi watu kujitokeza uwanjani.
  “Nadhani Waganda wamesononeshwa na matokeo ya timu yao kutofuzu Fainali za Mataifa ya Afrika dakika za mwishoni, hii kwa kweli imewafanya wapoteze hamu na mpira kidogo,”alisema.
  Uganda ilifungwa 1-0 na Zambia katika mechi ya kwanza ya Raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza fainali za mwakani za Mataifa ya Afrika na katika marudiano nayo ikashinda 1-0 nyumbani, kabla ya kutolewa kwa penalti.
  Hii ilikuwa mara ya pili mfululizo kwa Uganda kuzikosa fainali za AFCON dakika za mwishoni, kwani hata kuelekea fainali zilizopita mwaka jana Equatorial Guinea na Gabon, ilikomolewa na Kenya katika mechi ya mwisho nyumbani.
  Kundi A, linatarajiwa kuhitimisha mechi zake leo, kwa wenyeji na mabingwa watetezi, Uganda, The Cranes kucheza na Sudan Kusini, saa 12:00 jioni, mchezo ambao utatanguliwa na mechi kati ya Kenya, Harambee Stars na Ethiopia Uwanja wa Mandela.
  Kesho, saa 8:00 mchana, Tanzania Bara itamenyana na Somalia Lugogo na baadaye saa 10:00, Rwanda itacheza na Eritrea wakati keshokutwa, Sudan itaanza na Burundi saa 8:00 mchana na baadaye saa 10:00 jioni Malawi watamenyana na Zanzibar Lugogo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: STARS NA SOMALI KUCHEZA UWANJA KAMA WA LEADERS TU DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top