• HABARI MPYA

  Ijumaa, Novemba 30, 2012

  KAVUMBANGU AANZA KUWAZINGUA YANGA, GUMBO NAYE AENDELEA KUSUSA

  Kavumbangu

  Na Prince Akbar
  KIUNGO Rashid Gumbo na mshambuliaji Didier Kavumbangu ni wachezaji pekee wa Yanga, ambao hawajaanza mazoezi baada ya mapumziko mafupi ya wiki mbili na hawana sababu.
  Habari kutoka ndani ya Yanga, zimesema kwamba wachezaji wote ambao hawapo kwenye timu zinazoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge wanaendelea na mazoezi Uwanja wa sekondari ya Loyola, Dar es Salaam kasoro watano.
  Wachezaji ambao hawapo mazoezini pamoja na Gumbo na Kavumbangu, ni mabeki Ladislasu Mbogo, David Luhende na kiungo Shamte Ally.
  Imeelezwa Shamte na Luhende ni wagonjwa, wakati Mbogo amekwenda kumuuguza mama yake, Mwanza. “Gumbo na Kavumbangu hawana sababu,”kilisema chanzo.
  Gumbo amekuwa akilalamikia kuwekwa benchi na kuna wakati alifikia pia kusema anataka kuondoka kwenda timu ambayo atakuwa anacheza.
  Kavumbangu yuko kwenye mpango wa kuuzwa Qatar, lakini bado hiyo haiwezi kuhusiana na kutohudhuria kwake mazoezi.
  Yanga imepanga kufanya ziara ya mafunzo nchini Uturuki mwishoni mwa Desemba na mwanzoni mwa Januari mwakani, kabla ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mjini Kigali, Rwanda.   
  Mabingwa hao mara tano wa Kagame, 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012, wamepania kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu kurejesha heshima yao na wamewekeza kwenye maandalizi mazuri kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi hiyo.
  Yanga ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa inaongoza kwa pointi zake 29, ikifuatiwa na Azam yenye 24, wakati mabingwa watetezi Simba SC wana pointi 23.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KAVUMBANGU AANZA KUWAZINGUA YANGA, GUMBO NAYE AENDELEA KUSUSA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top