• HABARI MPYA

    Thursday, November 29, 2012

    POULSEN HAJAKATA TAMAA, ALIA NA BAHATI JANA

    Kim Poulsen jana

    Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
    KOCHA Mkuu wa timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen, raia wa Denmark, amesema kwamba bado ana matumaini ya kutinga Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge licha ya jana kuchapwa 1-0 na Burundi.
    Mbaya wa Kim na Stars jana, alikuwa mshambuliaji wa zamani wa Simba SC ya Dar es Salaam, Suleiman Ndikumana aliyefunga bao hilo dakika ya 52, katika mchezo huo wa Kundi B, uliofanyika kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya mechi ya jana, Poulsen alisema kwamba anaamini wakishinda mechi ya mwisho dhidi ya Somalia, watasonga mbele.
    Hata hivyo, Kim alisema haidharau Somalia kwani imeonyesha mchezo mzuri katika mechi zake zote mbili pamoja na kufungwa.
    “Nina muda mzuri kidogo wa kujiandaa na mchezo huo hadi Jumamosi, tutajiandaa vizuri na nina matumaini ya kushinda,”alisema.
    Akizungumzia mchezo wa jana, Kim alisema walitengeneza nafasi nyingi nzuri, lakini wakashindwa kuzitumia, mipira ikigonga mwamba na mingine ikiokolewa ikiwa inaelekea nyavuni, hivyo hana wa kumlaumu kwa matokeo hayo, bali habati haikuwa yao jana.
    Burundi walipata bao lao kwa penalti jana Nahodha huyo wa Burundi, anayechezea Inter Stars ya nyumbani kwao kwa sasa, akifunga baada ya yeye mwenyewe kuangushwa kwenye eneo la hatari na Shomary Kapombe.
    Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na Burundi walifanya mashambulizi mawili ya hatari zaidi, lakini sifa zimuendee ‘TZ One’, Juma Kaseja aliyeokoa hatari hizo.
    Stars hawakucheza soka yao ya chini kutokana na hali mbaya ya Uwanja, kujaa matope, kuwa wenye kuteleza kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kutwa nzima ya leo.
    Kipindi cha pili Stars walijitahidi kutaka kusawazisha mabao hilo, lakini bahati haikuwa yao na zaidi waliishia kukosa mabao mawili ya wazi.
    Kwa matokeo hayo, Burundi imeendelea kuongoza Kundi A, kwa pointi zao sita, mabao sita ya kufunga na moja la kufungwa, wakati Bara inabaki nafasi ya pili kwa pointi zake tatu, Sudan ya tatu ikiwa na pointi moja sawa na Somalia.
    Kikosi cha Stars jana kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe/Issa Rashid, Kevin Yondan, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Salum Abubakar, John Bocco, Mwinyi Kazimoto/Shaaban Nditi na Simon Msuva/Amri Kiemba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: POULSEN HAJAKATA TAMAA, ALIA NA BAHATI JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top