• HABARI MPYA

  Alhamisi, Novemba 29, 2012

  STARS WAOMBEWA VIAU VYA KUCHEZEA KWENYE MVUA KAMPALA

  Mashabiki wanaoiunga mkono Stars mjini hapa

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
  MASHABIKI wa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars waliopo hapa, wameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwatumia wachezaji wa timu hiyo viatu vya kuchezea kwenye mvua, kabla ya mechi ya mwisho ya Kundi B, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge Jumamosi.
  Wakizungumza baada ya mechi ya jana dhidi ya Burundi, ambayo Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, walichapwa 1-0 kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini mashabiki hao walisema hali ya hewa ya mji huu kwa sasa itaendelea kuwa ya mvua na TFF inapaswa kuchukua tahadhari baada ya matokeo ya jana.
  “Leo tumefungwa kwa sababu Uwanja ulikuwa unateleza kutokana na mvua na wenzetu Burundi walikuwa wana viatu vya mvua, kwa hivyo Uwanja haukuwasumbua, sasa na sisi lazima wachezaji wetu wapatiwe viatu hivyo,”alisema  Ally Abubakar aliyetoka River Side, Ubungo, Dar es Salaam kuja kuishangilia timu ya taifa.  
  Mbaya wa Stars jana, alikuwa mshambuliaji wa zamani wa Simba SC ya Dar es Salaam, Suleiman Ndikumana aliyefunga bao hilo dakika ya 52, katika mchezo huo wa Kundi B, uliofanyika kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole.
  Burundi walipata bao lao kwa penalti jana Nahodha huyo wa Burundi, anayechezea Inter Stars ya nyumbani kwao kwa sasa, akifunga baada ya yeye mwenyewe kuangushwa kwenye eneo la hatari na Shomary Kapombe.
  Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na Burundi walifanya mashambulizi mawili ya hatari zaidi, lakini sifa zimuendee ‘TZ One’, Juma Kaseja aliyeokoa hatari hizo.
  Stars hawakucheza soka yao ya chini kutokana na hali mbaya ya Uwanja, kujaa matope, kuwa wenye kuteleza kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kutwa nzima ya leo.
  Kipindi cha pili Stars walijitahidi kutaka kusawazisha mabao hilo, lakini bahati haikuwa yao na zaidi waliishia kukosa mabao mawili ya wazi.
  Kwa matokeo hayo, Burundi imeendelea kuongoza Kundi A, kwa pointi zao sita, mabao sita ya kufunga na moja la kufungwa, wakati Bara inabaki nafasi ya pili kwa pointi zake tatu, Sudan ya tatu ikiwa na pointi moja sawa na Somalia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: STARS WAOMBEWA VIAU VYA KUCHEZEA KWENYE MVUA KAMPALA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top