• HABARI MPYA

  Jumapili, Novemba 25, 2012

  NAHODHA SUDAN ATAKA JEZI YA YANGA HATA KESHO

  Hamisi Leon, Nahodha wa Sudan Kusini

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Sudan ya Kusini, Hamisi Leon amewataka viongozi wa Yanga waje Uganda katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge kushuhudia uwezo wake kwa mara nyingine.
  Mshambuliaji huyo wa Waw Salam ya Sudan Kusini, alikaribia kusajiliwa na Yanga Julai mwaka huu wakati wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, lakini akazidiwa kete na Didier Kavumbangu aliyekuwa anachezea Atletico ya Burundi.
  Hata hivyo, wakati huu ambao Kavumbangu yuko mbioni kuhamia Qatar anakotakiwa kwa dau zuri, Yanga ina nafasi ya kumsajili Leon.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY katika mahojiano maalum jana, Leon ambaye ni Nahodha wa Sudan Kusini alisema kwamba alifanya mazungumzo na Yanga alipokuwa Dar es Salaam na amekuwa na mawasiliano nao hata akiwa Sudan.
  Leon alisema kwamba anaipenda Yanga na atafurahi siku moja akijiunga nayo, kwani anaamini atacheza vizuri na kupata mafanikio makubwa.
  “Mimi ninajiamini nina uwezo na sibahatishi, nawaambia viongozi wa Yanga waje kuniona tena hapa Uganda, sijui kama watavutiwa na mshambuliaji mwingine zaidi yangu,”alisema Leon.
  Leon pamoja na kung’ara katika mchezo wa jana wa Kundi A, dhidi ya Ethiopia, lakini alishindwa kuiepusha timu yake na kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa wawakilishi hao wa CECAFA kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani Afrika Kusini.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: NAHODHA SUDAN ATAKA JEZI YA YANGA HATA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top