• HABARI MPYA

  Ijumaa, Novemba 30, 2012

  VIALLI AFUNGUKA, NI DOGO WA AZAM ALIYEIPIGIA MBILI ZANZIBAR JANA


  Vialli akishangilia baada ya kufunga bao la kwanza jana
  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
  KIUNGO wa Zanzibar, Khamis Mcha ‘Vialli’ amesema kwamba pamoja na kufunga mabao mawili jana, akiiwezesha timu yake kuilaza Rwanda 2-1 na kupanda kileleni mwa Kundi C, lakini hatakuwa na tamaa na tuzo ya ufungaji bora wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge, bali ataweka mbele maslahi ya timu.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa, Vialli alisema kwamba ikitokea nafasi ya kufunga atafanya hivyo, lakini kama wenzake watakuwa kwenye nafasi nzuri, atawapasia.
  “Ushindi wa leo ni matunda ya ushirikiano baina yetu kama timu nasi hatuna budi kuendeleza ushirikiano huu, kwa kuweka mbele maslahi ya timu,”alisema Vialli.
  Vialli jana aliifungIa mabao mawili Zanzibar Heroes, katika mchezo wa Kundi C, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge uliofanyika kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala.
  Kwa ushindi huo, Zanzibar Heroes imefufua matumaini ya kwenda Robo Fainali ya michuano hii, ikipanda kileleni mwa Kundi hilo, kwa pointi zake nne, Rwanda ikishuka nafasi ya pili kwa pointi zake tatu, sawa na Malawi, wakati Eritrea inashika mkia kwa pointi yake moja.
  Vialli alifunga mabao yake moja kila kipindi, la kwanza dakika ya sita na la pili dakika ya 61, yote akionyesha yeye ni fundi na mwenye akili na maarifa ya soka kutokana na kutulia na kumtungua kipa hodari kabisa katika ukanda huu, Jean Claude Ndoli.
  Rwanda ilipata bao lake kupitia kwa Dadi Birori dakika ya 79, ambaye aliingia uwanjani dakika ya 66 kuchukua nafasi ya Tumaine Ntamuhanga.
  Mchezo wa jana kama ulivyokuwa mchezo wa kwanza kati ya Malawi na Eritrea ulitibuliwa na mvua iliyoharibu mandhari ya Uwanja wa Mandela, hivyo haikuwa wa ufundi zaidi ya ‘butua butua’.
  Nahodha wa Zanzibar, Nadir Heroub ‘Cannavaro’ alisema baada ya mechi hiyo kwamba wamefuta makosa yao ya mchezo wa kwanza na sasa Wazanzibari wasubiri Kombe, wakati Haruna Niyonzima wa Rwanda, alilalamikia Uwanja mbovu leo kuwasababisha kucheza ovyo.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: VIALLI AFUNGUKA, NI DOGO WA AZAM ALIYEIPIGIA MBILI ZANZIBAR JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top