• HABARI MPYA

  Ijumaa, Novemba 30, 2012

  MUNGU SAIDIA KAPOMBE APONA KUWAZUIA WAZOMALI, AMIR MAFTAH NJE KESHO

  Kapombe mazoezini leo, akiwa mbele ya John Bocco

   Na Mwandishi wetu, Kampala
  KOCHA wa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amepata ahueni baada ya beki Shomary Kapombe kufanya mazoezi leo, kujiandaa na mechi ya kesho dhidi ya Somalia ambayo itakuwa ya mwisho ya Kundi B, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge.
  Kocha Poulsen amesema amefarajika mno kurejea kwa beki huyo wa kati wa Simba SC, ambaye aliumia katika mechi dhidi ya Burundi juzi.
  Daktari wa Stars, Dk Mwanandi Mwankemwa, amesema mchezaji mwingine majeruhi, Mwinyi Kazimoto hataweza kucheza kwa kuwa bado anaendelea kupata nafuu kwa hivyo wamemshauri kocha ampumzishe katika mechi ya kesho.
  Kocha huyo Mdenmark, amesema kwamba mechi ya kesho itakuwa ni ya kufa na kupona na kikosi chake kiko tayari kukamilisha kazi.
  Kocha huyo aliyasema hayo wakati Stars, inayodhaminiwa na Bia ya Kilimanajro Premium Lager, ikifanya mazoezi ya mwisho leo kabla ya mchezo wake na Somalia ili kukamilisha michezo ya Kundi B inayojumuisha Burundi, Tanzania, Somalia na Sudan.
  “Mechi hii ni sawa na kuwa na risasi moja na risasi hii unatakiwa kuitumia vizuri..ndio mtihani tunaokabiliwa nao katika mechi hii maana lazima tushinde ili tusinonge mbele katika mashindano haya,” alisema n akikosi chake kitapambana hadi dakika ya mwisho.
  Alisema ana imani na kikosi chake kwani wachezaji wote wana ari ya ushindi na kuendelea na mashindano kwani wameshaonesha kiwango kikubwa katika mechi mbili zilizopita huku Stars ikishinda mechi moja shidi ya Sudan na kufungwa nyingine na Burundi.
   “Katika mechi hii hakuna mchezo na nimeshawaambia wachezaji kabisa maana hapa ukifungwa unaondoka,” alisema.
  Meneja wa Bia ya Kilimanajro Premium Lager, George Kavishe alisema mechi hii ni muhimu kwa Stars na kuwaomba watanzania wanaoishi Kampala kujitokeza kwa wingi kuishangilia.
   “Vijana hawa wanahitaji sapoti kutoka kwa wadau wote  hasa katika mechi hii ya kesho itakayoamua kama Tanzania itafuzuu kuendelea au la….sisi tukiwa wadhamini wa timu tunafuatilia kwa karibu na tunawaomba Tanzania waishangilie na kuipa moyo timu yao,” alisema.
  Kikosi kinachotarajiwa kuanza katika mchezo huu dhidi ya Somalia ni Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Issa Rashid, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Amri Kiemba, John Bocco, Shaban Nditi na Salum Abubakary. Beki Amir Maftah hatacheza kwa sababu ana kadi mbili za njano.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: MUNGU SAIDIA KAPOMBE APONA KUWAZUIA WAZOMALI, AMIR MAFTAH NJE KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top