• HABARI MPYA

    Sunday, November 25, 2012

    AHADI HII IMEBEBA MUSTAKABALI WA HESHIMA YA ALHAJ MANJI YANGA


    KUNA wimbo mmoja wa Lady Jaydee unaitwa Siku Hazigandi na kwa wimbo huu pamoja na nyingine za mwanamuziki huyo wa kihistoria kuwahi kutokea nchini, daima nitaendelea kuwa mpenzi wa nyimbo zake.
    Na Mahmoud
    Bin Zubeiry
    Wimbo huu una maana pana sana- zaidi ya mtu yeyote anavyofikiria. Kama utatoa ahadi leo, kwamba mwakani utafanya kitu fulani hata kama hauna dhamira, tarajia hiyo siku itafika na ukweli au uongo wako utajulikana siku hiyo.
    Mimi wimbo huu huwa unanifariji sana kwamba, kama unakabiliwa na matatizo, mitihani ya dunia, usikate tamaa, siku hazigandi, ipo siku, siku za mashaka zitaisha na Mungu atakujaalia furaha tena.
    Kama unadharau watu kwa majaaliwa yako, basi fahamu siku hazigandi, ipo siku, siku zako za utawala zitakwisha nawe utaonja machungu ya dunia. Lady Jaydee aliimba.
    Juzi, Mwenyekiti wa Yanga, Alhaj Yussuf Mehboob Manji alisaini makubaliano ya awali na Kampuni ya Beijing Constructions Engineering Group iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Kaunda, unaomilikiwa na klabu hiyo.
    Manji alisaini makubaliano hayo na Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo, David Zhang, mbele ya Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam.
    Katika makubaliano hayo, ujenzi huo wa Uwanja utakaokuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 hadi 40,000 utaanza rasmi Juni mwakani.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa kusaini makubaliano hayo juzi mchana, Alhaj Manji alisema kwamba wanafurahi kuanza safari ya ujenzi wa Uwanja wao na anaamini huo ni mwanzo wa mzuri wa mipango yao ya kuifanya Yanga ijitegemee kiuchumi.
    Katika hatua nyingine, Manji alisema kwamba katika mipango yao ya kuifanya Yanga ijimudu kiuchumi, wanafikiria kulikarabati pia jengo dogo la klabu hiyo, liliopo Mtaa wa Mafia.
    Alhaj Manji alisema kesho kampuni hiyo ya ujenzi kutoka China, ambayo ndiyo iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachukua vipimo kwenye Uwanja wa Kaunda na Uongozi wa Yanga kuliwasilisha suala la ujenzi huo kwenye Mkutano Mkuu wa Wanachama wa klabu hiyo, Desemba 8, mwaka huu.
    Alisema baadhi ya fedha kwa ajili ya uwanja huo wa kisasa watakapo benki na gharama nyingine zitatokana na michango ya wanachama baada ya kuwa wamepata gharama nzima za ujenzi za uwanja huo.
    Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Beijing Constructions Engineering Group alisema wanafurahia kufikia makubaliano ya awali ya ujenzi wa uwanja na klabu ya Yanga.
    Alisema wao ndio walijenga Uwanja wa Taifa na viwango vya ujenzi vya uwanja huo vilisifiwa na timu ya taifa ya Brazil iliyokuja kucheza mechi ya kirafiki na Tanzania mwaka 2010 ikiwa njiani kuelekea Afrika Kusini ambako fainali za kombe la Dunia zilifanyika.
    Wakati naihariri habari kuhusu makubaliano hayo, nilikumbuka tukio la Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage kusaini mkataba na Waturuki kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa klabu yake.
    Leo ni zaidi ya mwaka sasa tangu Rage asaini makubaliano hayo, lakini habari iliyopo, hata hicho kiwanja kwa ajili ya kuujenga Uwanja huo, bado hawajakamilisha malipo yake.
    Maana yake nini? Ilikuwa ni kuwahadaa wanachama wa Simba au? Atajua mwenyewe Rage, lakini kwa vyovyote leo anaumbuka mwenyewe kwa sababu siku zimepita, hazikuganda na wana Simba bado hawana ndoto za kuwa na Uwanja wao chini ya Mwenyekiti huyo mwenye asili ya Kisomali.
    Nilicheka sana ‘juzi juzi’ alipoibuka na ahadi ya kuipeleka timu Ulaya kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani. Nikasema, haya shauri yake, hajajua tu siku hazigandi!
    Tuachane na ya Rage, huyu tumekwishamzoea mzee wetu. Hiyo ndio starehe yake na bila shaka hata yeye mwenyewe anajijua kama watu wanamjua desturi yake, sema mkavu tu babu huyu!
    Manji si Mwenyekiti wa kwanza wa Yanga kutoa ahadi ya kujenga Uwanja wa Kaunda na wakati kesho mkandarasi anakwenda kufanya vipimo, nataka niwakumbushe tu wasomaji wangu, wakati Tarimba Abbas, Francis Kifukwe wakiwa viongozi wakuu wa klabu hiyo, walikwenda wakandarasi kupima Jangwani.
    Huo ni wakati ambao haijafikiriwa kama iko siku itatokea timu inaitwa Azam FC na leo klabu hiyo ina miaka sita, lakini Uwanja wa Kaunda upo kama alivyouacha marehemu Tarbu Mangara, tena umezidi kuchakaa kwa kukosa japo matunzo tu.
    Azam FC leo ina Uwanja wa maana na akademi, ambayo hadi Mwanasoka Bora wa zamani Afrika, Abedi Ayew Pele alipozuru nchini aliusifia.
    Nina kila sababu ya kumuamini Manji, kwa sababu kila ukiitazama Yanga ya leo, bila ya yeye sijui ingekuwaje.
    Manji aliingia Yanga mwaka 2006 baada ya jitihada zilizofanywa na wanachama wa klabu hiyo akina Theonist Rutashoborwa (sasa marehemu), Mzee wa Mpunga, Mawakili Lugaziya na Matunda na baadhi ya Waandishi wa Habari za michezo wenye mapenzi na klabu hiyo, kuanzisha harambee ya Saidia Yanga, kufuatia hali mbaya ya kiuchumi kukithiri ndani ya klabu hiyo, chini ya uongozi wa Francis Kifukwe.
    Katika kutafuta misaada ya kuibeba timu wakati huo ipo kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame ndipo wakampata Manji naye kwa mapenzi yake, akasema; “Nitaubeba mzigo wote”, na kweli hadi leo, amekuwa akiilea Yanga tangu kama mfadhili hadi sasa Mwenyekiti.
    Hadi sasa, Manji ameingia kwenye historia Yanga kama miongoni mwa watu muhimu kuwahi kutokea kwenye klabu hiyo, bila hata ya ahadi ya Uwanja.
    Naandika makala haya kwa sababu kwa uzoefu wangu, Manji ana desturi ya kususa anapopata upinzani kidogo kutoka kwa watu wenye mlengo tofauti naye.
    Amewahi kususa zaidi ya mara mbili na kuifanya Yanga iyumbe kidogo- wakati Wakili Imani Madega na Lloyd Nchunga wakiwa viongozi wa Yanga.
    Na Manji atarajie akiwa Mwenyekiti wa Yanga, lazima ataendelea kukabiliana na upinzani kwani hiyo ndiyo demokrasia katika vitu ambavyo vinagusa hisia za wengi.
    Hivyo basi, hata wazo lake la ujenzi wa Uwanja, si ajabu wakatokea ‘maputo’ washajazwa upepo wakaanza kulipinga na kumzulia Mwenyekiti wao mambo.
    Manji ajiandae kwa lolote, ili mradi tu ahakikishe anatimiza ahadi ambayo kwa sasa baadhi ya wana Yanga wanalala macho wakiomba Juni 2013 ifike kijiko kishuke Jangwani kuchimba.
    Tofauti na kutimiza ahadi hiyo, hakika Manji atajishushia heshima yake kwa kiasi kikubwa mbele ya wana Yanga na jamii ya Watanzania kwa ujumla.
    Na mashabiki ni watu ‘hawana adabu’, wanaweza kuthubutu hata kumfananisha na Rage. Hivyo basi, Manji ajue kwamba, ahadi ya ujenzi wa Uwanja wa Kaunda, imebeba mustakabali wa heshima yake.  Wasalam!
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: AHADI HII IMEBEBA MUSTAKABALI WA HESHIMA YA ALHAJ MANJI YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top