• HABARI MPYA

  Jumatano, Novemba 28, 2012

  OKWI ASEMA KOCHA ALIWAAMBIA WASITUMIE NGUVU NYINGI JANA

  Okwi

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
  EMMANUEL Okwi, mshambuliaji wa Uganda, The Cranes amesema jana kocha wao Bobby Williamson, raia wa Scotland aliwalekeza kucheza bila kutumia nguvu nyingi, ili kutunza nguvu kwa ajili ya mechi zijazo na ndiyo maana walipata ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Ethiopia katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker, Challenge.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Mandela, Namboole, Okwi anayechezea Simba SC ya Tanzania, alisema kwamba kocha wao alitaka washinde bila kutumia nguvu nyingi, kwa kuwa mashindano bado yapo katika hatua za awali.
  “Ni kweli bado mapema sana, mtu ukitumia nguvu nyingi unaweza kuumia na kuiachia timu pengo, sasa kocha amekuwa makini sana na sisi tunafuata maelekezo yake. Na amekuwa mwoga baada ya Abbel Dhaira (kipa) kuumia kwenye mechi na Kenya,”alisema Okwi na kuongeza.
  “Na ukiangalia ni kweli, haina maana kuingia Robo Fainali wakati wachezaji wako wengi majeruhi, hautafika mbali, na sisi lengo letu ni kutetea Kombe hapa, tena mashindano yanafanyika nyumbani,”alisema Okwi.
  Uganda jana ilishinda 1-0 na sasa inaongoza Kundi hilo kwa pointi zake sita, mabao mawili ya kufunga, haijafungwa bao hata moja, ikifuatiwa na Kenya yenye pointi tatu, mabao mawili ya kufunga na moja la kufungwa, Ethiopia pointi tatu pia bao moja la kufunga na moja la kufungwa na Sudan Kusini ambao hawana pointi wanashika mkia. Matokeo hayo yanamaanisha Uganda tayari imefuzu Robo Fainali, wakati Kenya na Ethiopia japo zina nafasi kubwa, lakini kwa uhakika zaidi ni hadi matokeo ya mechi za mwisho za kundi hilo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: OKWI ASEMA KOCHA ALIWAAMBIA WASITUMIE NGUVU NYINGI JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top