• HABARI MPYA

  Jumanne, Novemba 27, 2012

  ZANZIBAR WAOMBA RADHI KWA SARE YA JANA


  Wachezaji wa Zanzibar baada ya mechi jana
  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
  NAHODHA wa Zanzibar, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amewaomba radhi mashabiki wa soka wa Zanzibar kwa kushindwa kuifunga Etritrea jana na kuahidi watafanya vizuri katika michezo ijayo.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY mjini hapa, beki huyo wa Yanga alisema kwamba matokeo ya jana yaliwasononesha mno na hawakuyatarajia kabisa, na ndiyo maana baada ya mchezo wachezaji wote walikuwa wenye huzuni.
  “Kwa kweli hatukutarajia kabisa, na hatuwezi kumlaumu mtu yeyote, sisi wenyewe tu hatukucheza vizuri. Hayo ni mambo ambayo yanatokea kwenye soka,”alisema.
  Cannavaro alisema kwamba si kweli kama waliwadharau Eritrea, hapana bali ilitokea tu hali ya wao kutokuwa vizuri kimchezo.
  “Tulikuwa tunajiamini na tuna uzoefu na Eritrea, ni timu inayosumbua sana, lakini leo (jana) mipango yetu yote waliinasa, inatokea hiyo kwenye mchezo, tunawaomba radhi mashabiki wetu nyumbani na tunaomba waendelee kutusapoti na kuwa na imani na timu yao,”alisema.
  Cannavaro alisema wamejifunza kutokana na makosa ya jana na baada ya mechi kila mchezaji alisema kuna kazi ya kufanya. “Tumekubali wote, kuna kazi ya kufanya, na kweli tutafanya kazi kweli, tunajua mechi zote zilizobaki ni ngumu, lakini tutapigana,”alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: ZANZIBAR WAOMBA RADHI KWA SARE YA JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top