• HABARI MPYA

    Sunday, November 18, 2012

    HUU NDIO MSINGI WA TIMU BORA YA TAIFA BAADAYE NA HAPA NDIPO PA KUSHIKIA


    MARA kadhaa nimeandika juu ya umuhimu wa kuwekeza katika soka ya vijana, ili kutengeneza msingi wa timu bora ya taifa ya baadaye.
    Na Mahmoud Bin Zubeiry
    Kwa wasomaji wangu wazuri, bila shaka watakuwa wanakumbuka namna nilivyokuwa nashauri kuhusu maandalizi ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys tangu hata Kenya na Misri hazijajitoa.
    Pamoja na uzito wa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hatimaye dakika za mwishoni wakafanikiwa kuiwekea mikakati timu hiyo, kwa kuiundia Kamati Maalum ya kuisaidia, chini ya Mwenyekiti, Ridhiwani Kikwete na Wajumbe kama Kassim Dewji, Abdallah Bin Kleb, Seif Ahmad Magari, Nassor Bin Slum, Salim Abdallah na wengineo.
    Katika kipindi kifupi cha kuundwa kwake, Kamati hiyo imeonyesha ufanisi na hadi leo Serengeti Boys inaingia kwenye mchezo wa kwanza wa Raundi ya tatu na ya mwisho dhidi ya Kongo Brazzaville Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuna matumaini.
    Yapo matumaini ya timu hiyo kukata tiketi ya kucheza Fainali za U17 Afrika mwakani nchini Morocco.
    Juzi, nilihudhuria hafla ya chakula cha usiku cha kuchangia timu hiyo, ambayo hata hivyo haikufanikiwa kutokana na kuchelewa kwake kuanza, wadau wengi walioalikwa waliondoka baada ya kuona muda walioambiwa shughuli itaanza unazidi kuyoyoma na hakuna dalili za kuanza kwake.
    Lakini angalau unaweza kuona Wajumbe wanafanya kazi ndani na nje ya Uwanja, kuhakikisha timu hiyo inafuzu.
    Hakuna asiyefahamu kwamba nyumba bora inatokana na msingi wake imara- hivyo hata soka ya Tanzania, inatakiwa kujengewa msingi imara, ambao ni kuwekeza kwenye soka ya vijana.
    Jamani, kuwekeza kwenye soka ya vijana si tu kuanzisha vituo au timu za vijana, bila kuwa na mikakati ya kuwaendeleza vijana wenyewe hatua kwa hatua.
    Tustaajabu kwa nini Tanzania haijacheza tena Fainali za Mataifa ya Afrika tangu ilipofuzu kizalizali mwaka 1980, ikiwa hatuna msingi imara wa soka ya vijana?
    Lazima tuzoeleke kwenye Fainali za Afrika za Vijana, ili tufikirie kucheza Fainali za wakubwa.
    Niliwahi kutoa mfano mdogo tu; Mchezaji anapigiwa wimbo wa taifa akiwa kwenye fainali za vijana za Afrika, tarajia huyo lazima atatamani kupigiwa wimbo huo na kwenye fainali za wakubwa pia.
    Juzi, maneno ya Nahodha wa Serengeti, Miraj Adam na Msaidizi wake, Hussein Twaha yalionyesha dalili hizo, vijana wamefurahia hadhi tu waliyopewa kwa kuundiwa Kamati ya kuwasapoti na wameahidi kuifunga Kongo leo.
    Wamehamasika, tayari wana hamu na kitu. Lakini kama wangetelekezwa tu kama ilivyokuwa, bila kuonyeshwa kwamba kuna watu wapo nyuma yao, leo dhamira ingekuwa kushindana kwa uwezo na nguvu zao zote, au kucheza kutimiza wajibu?
    Soka yetu inazidi kuporomoka kila kukicha- leo Tanzania ni ya 134 kwa ubora katika viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), yaani hata katika ukanda wetu wa CECAFA, tunazwazidi Somalia (193), Sudan Kusini (200) na Eritrea tu (192), lakini nchi nyingine zote, Uganda (86), Ethiopia (102), Sudan (102), Rwanda (122), Burundi (128) na Kenya 130 zinatuzidi.
    Tangu Jakaya Kikwete aingie Ikulu, tumekwishabadilisha walimu watatu wa kigeni, Mbrazil Marcio Maximo ambaye chini yake tulikosa fainali mbili za Afrika, zilizofanyika Ghana 2008 na Angola 2010, Mdenmark Jan Borge Poulsen ambaye chini yake tulikosa tiketi ya Gabon na Equatorial Guinea na huyu wa sasa Kim Poulsen, ameshindwa kutupa tiketi ya Afrika Kusini mwakani.
    Hakuna matarajio ya mabadiliko makubwa hata baada ya miaka 20 ijayo, iwapo staili zitaendelea kuwa hivi hivi na umefika wakati sasa tukakubali kujiwekea dira mpya ya muda mrefu.
    Lazima tukubali kuwekeza gharama katika kuwaandaa wachezaji kwa muda wa kutosha, ili baadaye tuwe na timu nzuri ya taifa, timu ya ushindani.
    Mara kadhaa nimekuwa nikirudia kushauri juu ya umuhimu wa kuzishirikisha timu zetu za vijana kwenye mashindano ya kimataifa kwa ukamilifu, lakini bado wahusika hawajaona umuhimu wa hilo.
    Kwa sasa Tanzania kuna mashindano mengi ya vijana ambayo yanasaidia kuibua vipaji, lakini tatizo hakuna mfumo wa kuwaendeleza hao vijana, matokeo yake inakuwa sawa na mkulima anayepanda mazao yake, lakini anashindwa kuyatunza, je, huyo atavuna kweli? Hicho ni kilimo cha aina yake.
    TFF wanapaswa kutenga bajeti na mikakati madhubuti kwa ajili ya timu za vijana chini ya umri wa miaka 17, 20 na 23 - kwani hilo ndilo chimbuko la kuwa na timu bora ya taifa baadaye.
    Nitatoa mfano; Julai 8, mwaka 2001, Ghana iliingia fainali ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 na ikafungwa 3-0 na Argentina kwenye Uwanja wa Jose Amalfitani mjini Buenos Aires, mabao ya Diego Colotto dakika ya sita, Javier Saviola dakika ya 14 na Maxi Rodriguez dakika ya 73.
    Kikosi cha Ghana siku hiyo kilikuwa; Maxwell Banahene, Sulley Muntari, Michael Essien, Patrick Villars, Emmanuel Pappoe, Ibrahim Abdul Razak, Razak Pimpong aliyempisha Frank Osei dakika ya 75, Derek Boateng, John Mensah, John Pantsil na Kwaku Duah, aliyempisha Samuel Thompson dakika ya 68.
    Mwaka 2006 tukashuhudia asilimia kubwa ya vijana hao na wengine walioibuliwa baadaye wakiiwezesha Ghana kukata tiketi ya kucheza fainali za Kwanza za Kombe la Dunia nchini Ujerumani.
    Oktoba 6, mwaka 2009, Ghana ilitwaa Kombe la Dunia la vijana chini ya umri wa miaka 20, ikiifunga Brazil katika fainali kwa mikwaju ya penalti 4-3, baada ya dakika 120 za bila kufungana, kwenye Uwanja wa Cairo International, Cairo.
    Kikosi cha Ghana kilichoweka rekodi ya kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, kilikuwa; Daniel Adjei, Samuel Inkoom, Jonathan Mensah, Daniel Addo, David Addy, Abeiku Quansah aliyempisha Opoku Agyemang dakika ya 107, Emmanuel Agyemang-Badu, Nahodha Andre Ayew, Mohammed Rabiu aliyempisha
    Bright Addae dakika ya 101, Ransford Osei aliyempisha Ghandi Dassenu dakika ya 65 na Dominic Adiyiah.
    Tumeona mwaka juzi, mseto wa nyota walioifikisha fainali ya U20 Ghana na walioipa ubingwa wa michuano hiyo 2009 Misri, ukiifikisha timu ya wakubwa ya nchi hiyo Robo Fainali ya Kombe la Dunia.
    Ghana ingeweza kuweka historia ya kuwa nchi ya kwanza kufika Nusu fainali, kama si refa Mreno Olegario Benquerenca kutoa uamuzi wa utata, baada ya Luis Suarez wa Uruguay kuupangua mpira uliokuwa tayari nyavuni.
    Nimetoa mfano kwa Ghana, kwa sababu ndio ambao kwa miaka ya karibuni wamevuna matunda ya kuwekeza kwenye soka ya vijana- lakini kwa ujumla nchi zote duniani zilizo makini katika soka zinatilia mkazo soka ya vijana.
    Sasa Mungu katusaidia, tumepata sehemu ya kutengenezea msingi imara, ambao ni kuhakikisha Serengeti inakwenda Morocco mwakani. Binafsi nimefurahi sana na ninatarajia furaha zaidi kuanzia leo kutoka kwa vijana hao. Tujitokeze kwa wingi kwenda kuwashangilia vijana, ili kuwapa hamasa washinde. Mungu ibariki Tanzania. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: HUU NDIO MSINGI WA TIMU BORA YA TAIFA BAADAYE NA HAPA NDIPO PA KUSHIKIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top