• HABARI MPYA

  Jumatano, Novemba 28, 2012

  KOCHA ATAJA SABABU MOJA TU YA KUMTEMA BABBI KIKOSINI ZANZIBAR HEROES

  Abdi Kassim 'Babbi'

  Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
  KOCHA wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, Salum Bausi Nassor amesema kwamba amemtema katika timu hiyo, kiungo mkongwe Abdi Kassim Sadallah ‘Babbi’ kwa sababu ameongezeka uzito na amekuwa mzito sana.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana Uwanja wa Mandela, Namboole, Bausi alisema kwamba Babbi anatakiwa kupambana na uzito ili arejeshwe Zanzibar Heroes.
  “Kama unavyoona, haya mashindano yamekuwa ya kasi sana sasa, na Babbi amekuwa mzito sana na hata huko Azam, anaingizwa dakika 20 za mwisho, lazima uwe na wachezaji wenye kasi, wewe mwenyewe umeona mechi na Eritrea ilivyokuwa ngumu,”alisema.
  Awali ya hapo, jana kipa namba moja wa Uganda Abbel Dhaira alisema kwamba anavutiwa sana na uchezaji wa Babbi pamoja na wachezaji wengine, Mrisho Ngassa wa Tanzania Bara na Haruna Niyonzima wa Rwanda.
  “Hao ni wachezaji ambao napenda sana kuwatazama, nasikia Babbi hajaja, sijui kwa nini, kocha wao anajua, ila yule mchezaji mzuri sana, anapiga sana mashuti, ana nguvu, ananivutia, namjua vema,”alisema Dhaira.
  Zanzibar juzi ilianza kwa sare michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge inayoendelea mjini hapa, baada ya kutoka 0-0 na Eritrea katika mchezo wa Kundi C.
  Matokeo hayo yanawaweka katika wakati mgumu kuweza kuendelea na mashindano haya na sasa wanatakiwa kupambana zaidi katika mechi zao mbili zijazo ili washinde na kutinga Robo Fainali.
  Nahodha wa Heroes, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ pamoja na kuwaomba radhi Wazanzibari kwa sare hiyo, lakini pia ameahidi watajituma na kufanya vizuri katika mechi zijazo.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments
  Item Reviewed: KOCHA ATAJA SABABU MOJA TU YA KUMTEMA BABBI KIKOSINI ZANZIBAR HEROES Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top