• HABARI MPYA

  Thursday, February 11, 2016

  YANGA SC SASA WABEBA NYOTE WOTE KWENYE ATC, WAKITOKA MAURITIUS DEGE LINAWASHUSHA PEMBA KWA MAWINDO YA KUUWA MNYAMA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  NDEGE ya Shirika la Ndege Tanzania (ATC) itaisafirisha Yanga SC kesho kwenda mjini Curepipe, Mauritius kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Cercle de Joachim. 
  Na Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ameamua kubeba kikosi chake chote, kwa kuwa baada ya mchezo huo Jumamosi, ndege hiyo ya ATC itaichukua timu hiyo kuipeleka Pemba, visiwani Zanzibar.
  Yanga SC itaweka kambi kisiwani Pemba, kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya mahasimu Simba SC, Februari 20, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Matheo Anthony naye anakwenda na timu Mauritius kesho

  Na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE inafahamu kikosi kitaondoka kesho asubuhi kwa ndege ya ATC huku kocha Pluijm akiwabeba pia, kipa Benedicto Tinocco, kiungo Godfrey Mwashiuya na mshambuliaji Matheo Anthony ambao awali ilikuwa waachwe. 
  Awali, Yanga SC ilipanga kuondoka nchini jana kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SA), ambalo hata lilishindwa kuwapatia ndege ya kuunganisha mapema mjini Johannesburg, kwenda Curepipe.
  Kwa sababu hiyo, Yanga SC ikaachana na SA na kuamua kukodi ndege ya ATC ili kuepuka kuwachosha wachezaji wake kwa safari ndefu.  
  Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumamosi kuanzia Saa 9:30 Alasiri kwa saa za Mauritius Uwanja wa Curepipe mjini Curepipe kabla ya timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye Dar es Salaam.
  Yanga SC leo asubuhi imefanya mazoezi yake ya mwisho kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam kabla ya safari kesho. 
  Mkuu wa Msafara anatarajiwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ayoub Nyenzi, wakati upande wa viongozi wanakwenda Katibu Mkuu, Baraka Deusdedit na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu, Jerry Muro.

  KIKOSI KINACHOKWENDA MAURITUS;
  Makipa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’ na Benedicto Tinocco.
  Mabeki; Juma Abdul, Mbuyu Twite (DRC), Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Vincent Bossou (Togo) na Pato Ngonyani.
  Viungo ni; Said Juma ‘Makapu’, Salum Telela, Thabani Kamusoko (Zimbabwe), Haruna Niyonzima (Rwanda), Simon Msuva, Issoufou Boubacar (Niger), Godfrey Mwashiuya na Deus Kaseke.
  Washambuliaji ni; Malimi Busungu, Paul Nonga, Amissi Tambwe (Burundi) na Donald Ngoma (Zimbabwe).

  BENCHI LA UFUNDI; 
  Kocha Mkuu; Hans van der Pluijm (Uholanzi)
  Kocha Msaidizi; Juma Mwambusi
  Kocha wa Makipa; Juma Pondamali
  Daktari; Nassor Matuzya
  Meneja; Hafidh Saleh
  Mchua Misuli; Jacob Onyango
  Mtunza Vifaa; Mohammed Mpogolo
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC SASA WABEBA NYOTE WOTE KWENYE ATC, WAKITOKA MAURITIUS DEGE LINAWASHUSHA PEMBA KWA MAWINDO YA KUUWA MNYAMA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top