• HABARI MPYA

  Tuesday, February 16, 2016

  AVEVA: MAZEMBE WAKO TAYARI KUTUPA MGAWO WA SAMATTA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Simba SC imesema kwamba ipo katika hatua nzuri ya kupata mgawo wao wa fedha za mauzo ya mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta, aliyeuzwa KRC Genk ya Ubeligi kutoka Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Simba SC ambayo ilimuuza Samatta klabu ya TP Mazembe mwaka 2012, inapaswa kupata asilimia 20 ya fedha ambazo TP Mazembe imelipwa baada ya kumuuza Samatta kwenye klabu hiyo ya Ubelgiji.
  Rais wa Simba SC, Evance Aveva, ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE kwamba tayari wamekwishawaandikia barua TP Mazembe ya kuwajulisha kuhusu na mgawo ambao wanastahili kupata kama moja ya klabu ambayo imemkuza Samatta kabla kutoka nje.
  Rais wa Simba SC, Evans Aveva (kushoto) amesema TP Mazembe wako tayari kuwapa mgawo wa mauzo ya Samatta

  Aveva amesema kutokana na hilo, baada ya kutuma barua kwa uongozi wa timu hiyo, umerejesha majibu ya kuwa mara baada ya kukamilisha taratibu zote za uhamisho wa mchezaji huyo na kulipwa mgawo wao, watahamia kwenye asilimia 20 ya Simba.
  "Sisi tumefanya taratibu zote zinazotakiwa kufanywa, na tumezungumza na TP Mazembe wametuomba tuvute subira kidogo, wakati wakikamilisha zoezi hilo,"alisema Aveva.
  Alisema hata hivyo wao kama Simba, hawana wasiwasi na suala hilo, kwa sababu limefikia mahala pazuri baada ya mazungumzo kufanyika baina ya pande zote mbili.
  Samatta alijiunga TP Mazembe mwaka 2012, akitokea Simba, kwa dau la dola za marekani 150,000, ambapo ameitumikia timu hiyo kwa mafanikio kwa kipindi cha miaka minne huku akiipa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika huku naye akishinda tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika Januari mwaka huu.

  Samatta akikabidhiwa jezi namba 77 wakati wa utambulisho wake baada ya kusaini KRC Genk

  Baada ya kufanya vizuri, Mazembe imemuuza Samatta KRC Genk kwa dola za Kimarekani 800,000 (zaidi ya Sh. Bilioni 1.7).
  Samatta tayari ameanza kuitumikia klabu yake mpya ya Genk kwenye michezo ya Ligi Kuu nchini humo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AVEVA: MAZEMBE WAKO TAYARI KUTUPA MGAWO WA SAMATTA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top