• HABARI MPYA

    Saturday, November 20, 2021

    YANGA CHUPUCHUPU KWA NAMUNGO, 1-1


    VINARA, Yanga SC wamepunguzwa kasi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kutoa sare ya 1-1 na wenyeji, Namungo FC jioni ya leo Uwanja wa Ilulu mjini Lindi.
    Namungo FC walitangulia kwa bao la mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa akiifunga timu yake ya zamani dakika ya 53, kabla ya kiungo Saido Ntibanzokiza kumfunga Mrundi mwenzake, kipa Jonathan Nahimana kwa penalti dakika ya 82.
    Yanga inafikisha pointi 16 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi mbili zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC baada ya timu zote kucheza mechi sita.


    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Geita Gold wamewachapa wenyeji, Kagera Sugar 2-1 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
    Mabao ya Geita yamefungwa na George Mpole yote dakika ya kwanza na 35, wakati la Kagera limefungwa na Mbaraka Yussuf dakika ya 11.
    Geita inafikisha pointi tano na kujiinua kidogo kutoka nafasi ya 15 hadi ya 13 kwenye Ligi ya timu 16, wakati Kagera Sugar inabaki na pointi zake nane katika nafasi ya sita baada ya wote kucheza mechi sita.
    Nayo Mbeya City imeshinda 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya. Mabao ya Mbeya City yamefungwa na Juma Luizio dakika ya 45, Juma Shemvuni dakika ya 60 na Suleiman Ibrahim dakika ya 85, wakati la Mtibwa limefungwa na Salum Kihimbwa dakika ya 82 kwa penalti.
    Kwa ushindi huo, Mbeya City inafikisha pointi 10 na kupanda nafasi ya tatu ikiizidi wastani wa mabao tu Polisi Tanzania baada ya wote kucheza mechi sita, wakati Mtibwa inabaki na pointi zake mbili za mechi sita sasa katika nafasi ya 14 kwenye Ligi ya timu 16.
    Mtibwa inazizidi wastani wa mabao tu Geita Gold na KMC zilizo chini yake mkiani kwenye eneo la kushuka moja kwa moja.
    Ikumbukwe timu zitakazomaliza nafasi ya 13 na 14 zitakwenda kumenyana na timu za Championship kuwania kubaki Ligi Kuu.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA CHUPUCHUPU KWA NAMUNGO, 1-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top