• HABARI MPYA

  Friday, November 19, 2021

  KAGERE APIGA MBILI, SIMBA YAICHAPA RUVU 3-1


  MABINGWA watetezi, Simba SC wameibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya wenyeji wa muda, Ruvu Shooting Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
  Mabao ya Simba yamefungwa na washambuliaji wa Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere mawili dakika ya 18 na 37 na Mtanzania mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kibu Dennis dakika ya 44, wakati la Ruvu limefungwa na Elias Maguli dakika ya 70.
  Mkongwe Erasto Nyoni aliikosesha Simba bao la nne dakika ya 72 baada ya mkwaju wake wa penalti kuokolewa na kipa wa Ruvu, Mohamed Makaka kufuatia Kibu Dennis kuangushwa na Michael Masinda kwenye boksi.
  Simba inafikisha pointi 14 baada ya mechi sita na kusogea nafasi ya pili, ikizidiwa pointi moja na watani, Yanga ambao pia wana mechi moja mkononi, wakati Ruvu inabaki na pointi sita za mechi sita ikishukia nafasi ya 11.
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, bao pekee la Benedictor Jaboc dakika ya 46 limewapa Coastal Union ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Polisi Tanzania Uwanja wa Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
  Coastal inafikisha pointi saba baada ya mechi sita na kusogea nafasi ya 10, wakati Polisi Tanzania inabaki na pointi zake 10 za mechi sita katika nafasi ya tatu.
  Nayo Tanzania Prisons imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Mbeya Kwanza Uwanja wa Mandela, Sumbawanga mjini Rukwa.
  Prisons inahama mkiani hadi nafasi ya 12 baada ya ushindi wa leo katika mchezo wa sita na Mbeya Kwanza inabaki na pointi zake saba za mechi sita, ikishukia nafasi ya saba kutoka ya sita.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAGERE APIGA MBILI, SIMBA YAICHAPA RUVU 3-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top