• HABARI MPYA

  Alhamisi, Agosti 25, 2016

  YAKIFANYIKA HAYA, TANZANIA ITAZOA MEDALI HATA 20 OLIMPIKI YA TOKYO 2020

  Na Jamal Malinzi, DAR ES SALAAM
  ⁠⁠⁠MICHEZO ya Olimpiki mwaka 2016 imemalizika mjini Rio de Jeneiro, Brazil huku Tanzania kwa mara nyingine ikirejea mikono mitupu.
  Lakini kama inavyofahamika, mwisho wa Olimpiki ya mwaka huu Rio, ndiyo mwanzo wa maandalii ya Olimpiki nyingine ya mwak 2020 mjini Tokyo, Japan.
  Kuna mambo matatu Tanzania inatakiwa kufanya kuhusu maandalizi ya MIchezo ya Olimpiki mwaka 2020 Tokyo.
  Kwanza ni maandalizi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23 (U-23)  kufaulu kushiriki fainali za Olimpiki 2020.
  Pili, ili timu ya soka na wanamichezo wengine wafaulu kushiriki na kushinda Medali za Olimpiki, zinahitajika fedha za maandalizi.

  Baadhi ya wachezaji wa timu ya Tanzania iliyoshiriki Michezo ya Olimpiki mjini Rio mwaka huu  

  Soka; TFF imeamua na kwa kuanza maandalizi ya mapema yenye kuonyesha matumaini ya kufuzu kucheza Olimpiki ya 2020 katika nafasi tatu za Afrika.
  Mwaka huu Afrika iliwakilishwa na Africa Kusini, Nigeria na Algeria. Nigeria wametutoa kimasomaso kwa kushinda Medali ya Shaba, wakati mwaka 1992 walishinda Fedha mjini Barcelona na 1996 walishinda Dhahabu nchini Marekani.
  Kiutaratibu, kwenye kufuzu ni timu za Taifa za vijana umri chini ya miaka 23 yaani U-23 zinatakiwa.
  Mwezi Desemba mwaka huu kutokana na ligi ya Taifa ya klabu za vijana chini ya umri wa miaka 20 inayoanza mwaka huu, tutakusanya kikosi cha awali cha timu ya Taifa U23 itakayoingia kambini.
  Hawa ni vijana waliozaliwa baada ya Januari 1, mwaka 1997 na utatumika utaratibu ule ule ulioutumia kuijenga timu imara ya U-17, Serengeti Boys kuhakikisha wanapata mazoezi, kambi na mechi za kimataifa za kujipima.
  Kufikia mwaka 2019 Tanzania itakuwa na kikosi imara cha soka (a world beating team) kitakachofuzu Olimpiki ya mwaka 2020.
  Kuhusu michezo mingine; Kwenye biashara kuna kitu kinaitwa niche. Tuangalie ni eneo gani Mungu ametupa karama kuliko binadamu wengine kisha tuweke nguvu hapo.
  Tanzania tuna uwezo mkubwa wa asili kwenye michezo ya  kukimbia, ngumi, kurusha mkuki na kurusha tufe. Hii inatutosha (kuogelea ). Tunapaswa kuamua kuwekeza kwenye kuandaa watu wa kwenda kucheza michezo hiyo Tokyo mwaka 2020 ili watuletee Medali.
  Tunapaswa kuanza kusaka vipaji kuanzia mwezi Desemba mwaka huu ili hadi kufika Juni mwakani tuwe na vijana wa kuanzia na tuwatafutie kambi nje ya nchi.
  Waende nje na kama ni masomo wakaendelee huko huko na walipiwe. Kama ni mabondia, waende kuweka kambi Cuba, wanariadha watafutiwe nyanda za juu waende, kama ni mbio fupi waende El Passo wakakae huko.
  Na tulipie hizi gharama, waende huko wakapikwe waive. Kama ni majaribio tuwalipie nauli watokee huko huko waende kwenye majaribio na warudi kambini.
  Tanzania tuna uwezo wa kuwashinda Wakenya, Waethiopia, Wamorocco na wengine ni suala la kuweka nia thabiti na kuwekeza.
  Yote haya yanahitaji mamilioni ya dola. Bila uwekezaji Medali zitaendelea kuwa ndoto.
  Tunatambua majukumu ya makubwa ya Serikali yetu katika kugharamia afya, elimu, ulinzi na usalama, kilimo, miundombinu na mengine na hatupaswi kuiongezea hili la gharama za  michezo.
  Tuna uwezo nalo. Huko nyuma niliwahi kushauri Baraza la michezo la Taifa (BMT) libadilishwe liwe Mamlaka ya Maendeleo ya Michezo (National Sports Development Authority na Shirika la  michezo ya kubahatisha lihamishiwe Wizara yenye dhamana  ya michezo.
  Chini ya utaratibu huu, itakuwa rahisi kutumia mapato yatokanayo na michezo ya kubahatisha katika kuandaa timu zetu za Taifa.
  Ukiwa na mpango mkakati mzuri, ukaanza kuutekeleza mapema na ukawa na fedha za uhakika za utekelezaji tusishangae 2020 Tanzania tukarudi na Medali si chini  ya 10 kutoka Tokyo.
  Ndiyo, tunaweza! Tuamue tu.
  (Mwandishi wa makala haya, Jamal Emil Malinzi ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF) 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YAKIFANYIKA HAYA, TANZANIA ITAZOA MEDALI HATA 20 OLIMPIKI YA TOKYO 2020 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top