• HABARI MPYA

  Jumanne, Agosti 23, 2016

  TAMBWE AFUNGA YANGA PUNGUFU IKILAMBWA 3-1 NA MAZEMBE LUBUMBASHI

  Na Mwandishi Wetu, LUBUMBASHI
  YANGA SC imehitimisha mechi zake za Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa mabao 3-1 na wenyeji TP Mazembe, Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, DRC.
  Kwa matokeo hayo, Mazembe inamaliza kileleni mwa Kundi A kwa pointi zake 13 baada ya mechi sita, wakati Yanga inamaliza mkiani kwa pointi zake nne. 
  Katika mchezo wa leo, Yanga ilicheza pungufu tangu dakika ya 30, baada ya beki wake chipukizi, Andrew Vincent Chikupe ‘Dante’ kutolewa kwa kadi nyekundu.
  Beki huyo aliyesajiliwa Mei mwaka huu kutoka Mtibwa Sugar alitolewa dakika mbili tu baada ya Mazembe kupata bao la kwanza lililofungwa na Jonathan Bolingi, aliyemalizia pasi ya Deo Kanda.
  Amissi Tambwe amefunga bao lake la pili kwenye Kombe la Shirikisho leo 

  Wakati Yanga SC wakikianza kipindi cha pili kwa kasi ya kusaka bao la kusawazisha, Mazembe wakafanikiwa kupata bao la pili, lililofungwa na Ranford Kalaba dakika ya 55 kabla ya Bolingi kufunga la tatu dakika ya 64.
  Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amissi Tambwe akaifungia Yanga SC bao la kufutia machozi dakika ya 75 – hilo likiwa bao la nne la timu hiyo kwenye mashindano hayo.
  Katika mabao hayo manne, Tambwe amefunga mawili, lingine kwenye mechi na MO Bejaia, wakati Mzimbabwe Donald Ngoma alifunga dhidi ya Medeama na mzalendo Simon Msuva akafunga kwa penalti Ghana.
  Yanga ilianza michuano hiyo kwa kufungwa 1-0 na MO Bejaia nchini Algeria, kabla ya kufungwa 1-0 tena na Mazembe na baadaye sare ya 1-1 na Medeama ya Ghana, mechi zote zikipigwa Dar es Salaam.
  Katika mzunguko wa pili, Yanga ikafungwa 3-1 na Medeama nchini Ghana, kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya Mo Bejaia Dar es Salaam na leo kupigwa 3-1 Lubumbashi.  
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite, Mwinyi Hajji Mngwali, Hassan Kessy, Andrew Vincent, Haruna Niyonzima, Thabani Kamusoko, Deus Kaseke/Matheo Anthony dk86, Said Juma ‘Makapu’/Oscar Joshua dk78, Amissi Tambwe na Simon Msuva/Juma Mahadhi dk68.
  TP Mazembe; Sylvain Gbohouo, Jean Kasusula, Joel Kimwaki, Djo Issama, Chirstian Luyindama, Solomon Asante, Christian Koffi, Daniel Adjei Nii, Ranford Kalaba/ Yaw Frimpong dk84, Deo Kanda/Adama Traore dk71  na Jonathan Bolingi/ Chavda Maisha  dk74.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TAMBWE AFUNGA YANGA PUNGUFU IKILAMBWA 3-1 NA MAZEMBE LUBUMBASHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top