• HABARI MPYA

  Jumanne, Agosti 30, 2016

  SAMATTA KUUNGANA NA STARS NIGERIA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta anatarajiwa kuungana na timu ya taifa nchini Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017).
  Taifa Stars inayofundishwa na mchezaji wake wa zamani, Charles Boniface Mkwasa inakwenda Nigeria kukamilisha ratiba tu, kwani tayari imekwishatupwa nje yam bio za Gabon, baada ya kufungwa 2-0 na Misri katika mchezo uliopita.
  Mkwasa alilazimika kumuacha kipa Deo Munishi ‘Dida’ aliyefiwa na baba yake mzazi Jumapili na kumchukua kinda wa JKT Ruvu, Said Kipao.
  Samatta anatarajiwa kuungana na Taifa Stars nchini Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kuwania tiketi ya AFCON 2017

  Kipao alimvutia Mkwasa baada ya kudaka vizuri Jumamosi kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara timu yake JKT Ruvu ikilazimisha sare ya 0-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Wachezaji wanaounda kikosi cha Stars ambacho kitaondokea kambini Hoteli ya Urban Rose mjini Dar es Salaam ni makipa Said Kipao – JKT Ruvu, Aishi Manula – Azam FC, Mabeki; Kevin Yondani, Vicent Andrew, Mwinyi Hajji Mngwali (wote Yanga SC), Mohamed Hussein 'Tshabalala' (Simba SC), Shomari Kapombe na David Mwantika (wote Azam FC).
  Viungo ni Himid Mao (Azam FC), Shiza Kichuya (Simba SC), Ibrahim Jeba (Mtibwa Sugar), Jonas Mkude (Simba SC), Muzamil Yassin (Simba SC), Juma Mahadhi (Yanga SC) na Farid Mussa (Tenerif, Hispania).
  Washambuliaji ni Simon Msuva (Yanga SC), Jamal Mnyate, Ibrahim Ajib (Simba SC), John Bocco (Azam FC) na 
  Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji).
  Mchezo huo baina ya timu zilizotoka sare ya 0-0 katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam mwaka jana utachezwa Septemba 3, mwaka huu mjini Lagos.
  Misri imemaliza mechi zake za Kundi G kwa kufikisha pointi 10, ikifuatiwa na Nigeria pointi mbili wakati Tanzania ina pointi moja. Chad ilizivurugia Nigeria na Tanzania baada ya kujitoa katikati ya mashindano kwenye kundi hilo na kuipa nafasi nzuri Misri kufuzu kiulaini. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA KUUNGANA NA STARS NIGERIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top