• HABARI MPYA

  Jumatatu, Agosti 29, 2016

  MECHI YA YANGA NA JKT RUVU YAAHIRISHWA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  MCHEZO wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Yanga SC na JKT Ruvu uliokuwa ufanyike Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam umeahirishwa.
  Habari ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE imezipata kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zimesema kwamba mchezo huo uliopangwa kuchezwa Jumatano ya Agosti 31 sasa utapangiwa tarehe nyingine.
  Na hatua hyo inatokana na Yanga kuomba uahirishwe kwa sababu ina wachezaji wengi katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
  Hao ni kipa Deogratius Munishi 'Dida', mabeki Vincent Andrew 'Dante', Kelvin Yondani na Mwinyi Hajji, kiungo Juma Mahadhi na mshambuliaji Simon Msuva.
  Aidha, Yanga pia imesema wachezaji wake wengine, beki Vincent Bossou (Togo), kiungo Haruna Niyonzima (Rwanda) na mshambuliaji Amissi Tambwe (Burundi) nao pia wameitwa na timu zao za taifa na kufanya idadi ya wachezaji wanane.
  Kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zinaruhusu timu ambayo wachezaji wake wasiopungua watano wameitwa timu za taifa kuahrishiwa mechi. 
  Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ ameita wachezaji 20 watakaosafiri kwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa kukamilisha ratiba ya mechi za Kundi G kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017).
  Mbali na Dida, Yondani, Dante, Mngwali, Mahadhi  na Msuva wengine ni Aishi Manula, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Shomari Kapombe (Azam FC) na David Mwantika (Azam FC).
  Viungo ni Himid Mao (Azam FC), Shiza Kichuya (Simba SC), Ibrahim Jeba (Mtibwa Sugar), Jonas Mkude (Simba SC), Muzamil Yassin (Simba SC), na Farid Mussa (Teneriffe ya Hispania).
  Washambuliaji ni Jamal Mnyate (Simba SC), Ibrahim Hajib (Simba SC), John Bocco (Azam FC) na Mbwana Samatta - CK Genk ya Ubelgiji.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MECHI YA YANGA NA JKT RUVU YAAHIRISHWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top