• HABARI MPYA

  Jumatano, Agosti 24, 2016

  SIMBA WATAKA BILIONI 1.2 ILI WAMRUHUSU KESSY KUCHEZEA YANGA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC jana imewasilisha rasmi pingamizi la usajili wa beki wake, Hassan Ramadhani Kessy kwa mahasimu, Yanga SC ikitaka ilipwe dola za Kimarekani 600, 000 zaidi ya Sh. Bilioni 1.2.
  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe aliiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana mjini Dar es Salaam kwamba wamewasilisha pingamizi na ushahidi wa kutosha kwamba Kessy alikiuka taratibu katika kuhamia kwake Yanga SC.
  “Hatuna wasiwasi katika hilo, tumejipanga kuifikisha hii kesi hadi FIFA, ili tu tupate haki yetu kama tulivyopata haki yetu kwenye kesi ya Okwi (Emmanuel),”alisema Hans Poppe jana. 
  Hassan Kessy (kushoto) ameingia katika mgogoro na Simba SC
  Wiki iliyopita, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kikao chake chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Richard Sinamtwa ilimruhusu Kessy kuecheza Yanga, lakini pia alipe fedha za kuvunja Mkataba wa Simba.
  Na jana Hans Poppe, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) alisema kwamba, katika Mkataba wao na Kessy walikubaliana atakayeuvunja atalipa dola za Kimarekani 600,000.
  Kessy alisajiliwa na Simba SC misimu miwili iliyopita kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa Mkataba wa miaka miwili akilipwa Sh. Milioni 20. 
  Kwa upande wake, Meneja wa Kessy, Athumani Tippo alisema anashangazwa na uamuzi wa Kamati kumtaka Kessy ailipe Simba wakati aliondoka baada ya kumaliza Mkataba.
  Tippo alisema Mkataba wa Kessy na Simba uliisha Juni 17 na beki huyo wa kulia akasaini Yanga SC Juni 21, baada ya kuzungumzo ya awali kufanyika mwishoni mwa Mei.   
  “Kilichotokea baada ya habari za Kessy kutaka kuhamia Yanga kuvuja, Mei 25 mwaka huu alipokwenda kwenye mechi ya fainali ya Kombe la TFF dhidi ya Azam mashabiki wakamvisha jezi ya Yanga,”.
  “Hakuvishwa na klabu ya Yanga, ni mashabiki. Sasa huwezi kusema Kessy alivunka Mkataba na Yanga kinyume cha utaratibu,”alisema Tippo.
  Pamoja na hayo, Tippo alisema kwamba amepeleka malalamiko Chama cha Wachezaji Tanzania (SPUTANZA) ili waweze kumsaidia mchezaji huyo katika sakata hilo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA WATAKA BILIONI 1.2 ILI WAMRUHUSU KESSY KUCHEZEA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top